Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
WAKATI watafiti kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiendelea kutafuta tiba ya kudumu ya UVIKO-19, idara ya chakula na dawa nchini Marekani imedhibitisha kuwepo kidonge(PICHANI JUU) kinachoweza kutibu ugonjwa huo na kuwa kimeonesha mafanikio makubwa dhidi ya kirusi kinacho sababisha UVIKO-19.
Kwa muujibu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (FDA) nchini Marekani, pamoja na mafanikio hayo, kampuni ya Merck nchini Marekani, iliyotengeneza dawa hiyo itatakiwa kupata michango kutoka kwa wataalamu nje ya shirika hilo kuhusu uwezekano wa madhara dhidi ya wajawazito pamoja na matatizo mengine katika kipindi cha ujauzito.
Mpaka Novemba 29, 2021 jumla ya watu 261,810,035 duniani wameripotiwa kupata maambukizi ya UVIKO-19 huku waliopona ni 236,468,381 na zaidi ya watu milioni 5,218,374 kupoteza maisha kwa mujibu wa mtandao wa https://www.worldometers.info/.
Katika taarifa iliyochapishwa na Associated Press (AP) ya Novemba 26, 2021, FDA walichapisha matokeo ya uchanganuzi wake wiki moja kabla ya kikao kinachokwenda kujadili uwezo wa dawa hiyo.
Hata hivyo FDA ilieleza uwezekano wa madhara ya dawa hiyo ambayo ni pamoja na sumu itakayoathiri mimba changa ambayo ni pamoja na kuzaliwa watoto wenye mapungufu, kutokana na majaribio ya dawa hiyo yaliyofanywa kwa wanyama.
Kutokana na matokeo hayo, imependekezwa kuwa katika mjadala unaotarajiwa kufanyika leo jumanne (30/11/2021), kuwa dawa hiyo isitolewe kwa wajawazito au kama ikibidi basi itolewe wakati ambao ni lazima sana kufanya hivyo, ikiwa ni pamoja na kuandikwa taadhari zote katika makasha ya dawa hiyo.
Kutokana na mashaka hayo, FDA ilisema kuwa, kampuni ya Merck imekubali kuwa dawa hiyo haitotumika kwa watoto wadogo.
“Madhara mengine ni madogo na hutokea mara chache huku ikionesha asilimia 2 ya wagonjwa hupatwa na kuharisha.” Imeeleza taarifa ya FDA.
More Stories
Dk. Mpango amwakilisha Samia sherehe za Uhuru wa Lesotho
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa
Waliombaka, kulawiti binti wa Yombo, Dar jela maisha