Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
LICHA ya leo Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutoa taarifa ya kumfungia miaka miwili na kumtoza faini ya Sh. milioni 8 aliyekuwa kocha wa Yanga Luc Eymael, wamebainisha kuwa maamuzi mengine dhidi ya kocha huyo pia yatapelekwa kwenye Shirikisho la Soka Duniani(FIFA).
Leo mchana, Kamati hiyo imetangaza kumfungia na kumpiga faini kocha huyo baada ya kumkuta na makosa mawili ikiwemo ubaguzi na udhalilishaji na tuhuma dhidi ya (TFF).
Kabla ya TFF kutangaza kuchukua adhabu kali kwa kocha huyo ikiwemo , tayari klabu yake ilishamfura kazi na kumtaka aondoke nchini haraka kutokana na mambo aliyoyafanya.
Sauti ya kocha huyo iliyodababisha kufukuzwa ilianza kusambaa siku moja kabla ya mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) waliocheza kwenye uwanja wa Samora, Iringa dhidi ya Lipuli ya Iringa ambao walipata ushindi wa goli 1-0 na kumaliza msimu wakiwa nafasi ya pili.
Katika sauti hiyo kocha huyo aliwatupia lawama waamuzi na kudai kuwaonea kwa kuwanyima penalti katika mechi zao kadhaa na kusema kuwa wapo kwa ajili ya Simba na si wao.
Kocha huyo amesema kuwa, Yanga hawatakaa watwae taji la Ligi kwani si klabu bora wala timu bora, hata viongozi wa klabu hiyo ni ziro na ndio maana waamuzi wanakuwa tofauti na wao kwakuwa ni masikini hawana njia nyingine ya kulikamata Shirikisho ambalo lipo kwa ajili ya Simba na sio Yanga hivyo wamruhusu aondoke kwani hataki kubaki ndani ya klabu hiyo.
“Sifurahii katika nchi hii, watu hawajasoma, sina gari, sina Wi-fi, kufanya kazi katika mazingira haya sio kwa ajili yangu kwani hata mke wangu hafurahii, kitu pekee ninachofurahia ni pale ambapo tunacheza viwanja vikiwa vimejaa mashabiki wetu ambao nao hawajui chochote kuhusu soka. Keleleza nao nawaona kama wapuuzi kama Nyani wanavyopiga kelele au Mbwa wanavyombweka,”.
Akizungumza hukumu hiyo, mjumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, Alex Mushumbusi amesema, wameridhika na ushahidi uliotolewa dhidi ya kocha huyo na atanza kutumikia adhabu hiyo kuanzia jana japokuwa kocha huyo ana haki ya kukata rufaa katika ngazi ya juu ambayo ni Kamati ya Rufaa ya TFF.
“Tuliwasiliana na Eymael ikiwemo kumtumia hukumu dhidi yake na kumpa wito wa kutakiwa kuhudhuria kikao cha kamati ya nidhamu kilichokutana Agosti Mosi lakini alijibu kuwa atatuma wawakilishi wake walioko Tunisia hivyo tukajiridhisha kuwa hakuwa na nia ya kuhudhuria kikao hicho na hivyo kuendelea na kusikiliza ushahudi wa upande wa mashataka,” amesema Mushumbusi.
Katika kosa la kwanza la kutoa maneno ya kibaguzi na udhalilishaji, Eymael amefungiwa kujihusisha na soka kwa miezi 24 (miaka miwili) na faini ya Sh. milioni 3 kwa mujibu wa bara ya 41(13) kanuni ya udhibiti wa makocha huku katika kosa la pili la kuituhumu TFF kuipendelea Simba, ametozwa faini ya Sh. milioni 5 milioni ikiwa ni kwa mujibu wa ibara ya 53(2) ya kanuni za nidhamu za TFF.
More Stories
Naibu Waziri wa Fedha abariki ujio mpya wa Bahati Nasibu
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes