Na Magreth Kinabo- Mahakama TEHAMA -2
MAHAKAMA ya Tanzania imesikiliza jumla ya mashauri 1,519 kupitia Mahakama Mtandao (Video Conferencing) kati ya Machi 23 hadi Aprili 21 mwaka huu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Jaji Mkuu wa Tanzania alilolitoa Machi 23 mwaka huu.
Katika agizo hilo aliitaka Mahakama kutumia Tekknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kupambana na ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa na virusi vya Corona.
Mkurugenzi Msaidizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Mahakama ya Tanzania (TEHAMA), Machumu Essaba alisema Mashauri hayo yamesikilizwa katika mahakama mbalimbali Jijini Dar es Salaam.
Akitaja idadi ya mashauri yaliyosikilizwa na Mahakama hizo, Essaba alisema Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilisikiliza na mashauri 424 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni mashauri 324.
Aidha, Mahakama za wilaya za Ilala, Temeke na Kigamboni zilisikiliza mashauri kama ifuatavyo; Ilala mashauri 465, Temeke 230. Mashauri hayo yalisikilizwa kutoka magereza ya Keko na Segerea.
Katika hatua nyingine, Essaba alisema Mahakama imeanza kutumia teknolojia maalumu inayomuwezesha Jaji kusikiliza kesi akiwa ofisini bila ya kufika katika chumba cha Mahakama ya wazi au chenye vifaa vya Mahakama Mtandao ‘Video Conference’.
Alisema teknolojia hiyo imeanza kutumiwa na Mahakama ya Tanzania ikiwa ni njia mojawapo ya kuepuka kuenea kwa maambukizi ya Virusi vya Corona. “Teknolojia hii inamwezesha Jaji kusikiliza kesi akiwa ofisini huku mhusika wa kesi akiwa katika chumba maalumu.
Utaratibu huu hauruhusu watu wengine kuwa katika vyumba hivyo, isipokuwa wahusika wa kesi, ambao ni Jaji na mleta maombi,’’alisema Essaba.
Aliongeza kuwa teknolojia hiyo inamwuwezesha Jaji kutumia kompyuta mpakato. Mahakama imeanza kutumia teknolojia hiyo Aprili 21, mwaka huu katika Mahakama ya Rufani Tanzania, ambapo Jaji wa Mahakama hiyo, Dkt. Gerald Ndika alisikiliza kesi, akiwa ofisini kwake jijini Dar es Salaam huku mleta maombi akiwa Mahakama Kuu Kanda Mwanza.
Hivyo teknolojia hiyo itakuwa inaendelea kutumiwa na Mahakama. Uongozi wa Mahakama katika kuunga mkono juhudi za Serikali kukabiliana na virusi vya Corona tayari imekabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Maafisa TEHAMA wa kanda 16 za Mahakama Kuu Aprili 21, mwaka huu ili kuziwezesha Mahakama nyingine kuanza kusikiliza kesi kwa njia ya Mahakama Mtandao.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja