Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli amepokea maombi ya wachimbaji wadogo wa Almasi katika Mji mdogo wa Maganzo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga na kuahidi kushughulikia kero zao endapo watamridisha tena madarakani.
Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa Mji mdogo wa Maganzo aliposimama kwa muda akiwa njiani kuelekea mkoani Simiyu na kusema Almasi imeletwa na mungu hivyo kila mtu ana haki ya kuchimba na hata Mji mdogo wa Maganzo umejengeka kutokana na madini hayo.
Akitoa maombi kwa rais Magufuli, mgombea ubunge katika Jimbo la Kishapu, Boniface Butondo ambapo amesema lipo eneo lenye madini ya Almasi ambalo limekuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya wachimbaji wadogo na mwekezaji Kampuni ya El- Hillal Minerals Ltd.
Butondo amesema, inadaiwa kuwa, mwekezaji huyo anamiliki eneo lenye zaidi ya ekari 2000 ambalo haliendelezi hivyo ni vyema Serikali ikatumia busara ione uwezekano wa kuwamegea wachimbaji wadogo wa almasi sehemu ya eneo hilo ili na wao waweze kujitafutia riziki.
“Mheshimiwa Rais mbali ya mafanikio tuliyoyapata ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita lakini tuna changamoto kadhaa ambazo tunaomba utusaidie kuzipatia utatuzi ikiwemo suala la wachimbaji wadogo wa Almasi wa hapa Maganzo ambao wamekuwa na mgogoro kati yao
na mwekezaji Kampuni ya El-Hillal Ltd,”.
“Mwekezaji huyo ana eneo katika kijiji cha Mwanholo ambalo haliendelezi, hivyo tunaiomba Serikali iangalie au itumie busara kuona jinsi gani wachimbaji wadogo wanaweza kupatiwa sehemu ya eneo hilo ili na wao waweze kujitafutia riziki,” ameeleza Butondo.
Akijibu ombi hilo Dkt. Magufuli amewaomba wachimbaji wadogo wafanye subira mpaka pale atakapokuwa amechaguliwa tena atayafanyia kazi maombi hayo kwa vile moja ya mambo yanayopewa kipaumbele na Serikali yake ni kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini hapa nchini.
“Ndugu zangu naomba mnivumilie tumalize uchaguzi, kikubwa hakikisheni mnanipatia kura nyingi mimi, wabunge na madiwani wote wanaotokana na CCM, mimi ni mtumishi wenu niachieni hili nitalifanyia kazi, lakini pia nikuombe mgombea ubunge wa hapa ukiapishwa
tu, hili liwe la kwanza kulishughulikia,” ameeleza Dkt. Magufuli.
Pia amewaahidi wakazi wa Mji mdogo wa Maganzo kwamba atakapochaguliwa tena na kuunda Serikali atahakikisha maeneo yote ya vijiji ambayo hayajapatiwa huduma ya maji ya kutoka Ziwa Victoria yanapatiwa huduma hiyo sambamba na kupatiwa umeme wa REA.
Kwa upande mwingine, aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Kishapu, Suleiman Masoud (Nchambi) ameahidi kumshika mkono mgombea ubunge anayechukua nafasi hiyo katika jimbo hilo, Boniface Butondo kuhakikisha anashinda kwa kishindo.
“Mheshimiwa Rais, naomba nikuhakikishie wewe na wanachama wote wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba pamoja na jina langu kutorejeshwa na vikao vya uteuzi, lakini sina kinyongo nitaendelea kushirikiana na wana CCM wenzangu kuhakikisha ushindi kwa mgombea wetu, ndugu Butondo,” amesema Nchambi.
More Stories
Tanzania,Uturuki kushirikiana kuinua sekta ya utalii nchini
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu