April 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simanjiro kusahau shida ya maji

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama wilayani Simanjiro itakuwa historia baada ya Serikali kujenga mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvu hadi Orkesumet wenye thamani ya Sh. bilioni 40.

Hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 89 za utekelezaji na unatarajiwa kuanza kufanya kazi kati ya mwishoni mwa mwezi huu Septemba au mwanzoni mwa Oktoba, 2020.

Mbali na mradi huo mkubwa, pia Serikali imetekeleza miradi mingine ya maji ikiwemo ya uchimbaji ya mabwawa ya kunyweshea mifugo ambayo tayari inatoa huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati akihutubia katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Orkesumet wilayani Simanjiro mkoani Manyara na kumuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na wagombea udiwani, Waziri Majaliwa ametaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo wa kutoa maji kutoka Mto Ruvu hadi Orkesumet wilayani Simanjio kuwa ni Irkujit ambapo tayari miundombinu ya maji imeshafika kijijini pamoja na Irkirungrung, Endonyongijape, Narosoito na Lorimorijoi.

Amesema miradi mingine inayotekelezwa katika Wilaya hiyo ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu vya maji 18 katika maeneo ya Kitwai, Msitu waTembo, Mirerani, Londrekes, Loibosoit, Kityangare Namalulu, Terrat, Olbili, Nadonjukin na Okutu. Ukarabati wa visima 13 umefanyika kikamilifu hatimaye vituo vya kuchotea maji vimefikia 95.

“Ujenzi wa bwawa la Narakauo kwa ajili ya matumizi ya mifugo na wananchi wa vijiji vya karibu yake unaendelea kupitia Wizara ya Mifugo kwa gharama ya sh. 413,865,700 sawa na asilimia 36,” amesema Waziri Majaliwa.

Pia amesema kuwa, mradi huo utakuwa mkombozi mkubwa kwa wafugaji wa ukanda wote wa Simanjiro ya juu na tayari Serikali imetumia Sh. milioni 412,724,300 kutekeleza mradi wa maji kutoka Nomokon hadi Narakauo ambao pia utasaidia kupunguza uhaba wa maji kwa wafugaji wa Kata nzima ya Loibosiret.

Licha ya utekelezaji wa miradi ya maji pia, Serikali imetenga milioni 500 kwa ajili kuboresha barabara za mjini katika Halmashauri ya Wilaya hiyo na zile za makao makuu ya Wilaya (Orkesumet) ambazo zinaendelea kuwekewa lami.

Akizungumzia kuhusu nishati ya umeme, Majaliwa amesema, kati ya vijiji 56 vya Wilaya ya Simanjiro, tayari vijiji 38 vimepata umeme na vijiji 18 visivyokuwa na umeme vitapatiwa nishati hiyo, na kuwataka wananchi hao waendelee kuwa na subira na kuiamini Serikali yao.

“Rais Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Simanjiro. Gharama za kuunganishiwa umeme huo zimepungua kutoka sh 177,000 hadi sh. 27,000,” amesema
Waziri Mkuu na kuongeza.

“Wananchi hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali”.