Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KOCHA mkuu wa klabu ya Yanga, Cedric Kaze ameweka wazi kuwa Winga wao Carlos Fernandes ‘Carlinhos’ bado anahitaji kupewa mazoezi zaidi yatakayomuwezesha kuhimili mechi za ushindani na mikiki mikiki ya dakika 90.
Mchezaji huyo amekuwa nje ya uwanja toka Oktoba 19 alipopata jeraha la enka akiwa mazoezi wakati timu yake inajiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Maafande wa Polisi Tanzania.
Tayari nyota huyo amesharudi uwanjani na juzi kwa mara ya kwanza chini ya kocha Kaze alikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kilichocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya African Lyon ambao walipata ushindi wa goli 3-1 zilizofungwa na Tuisila Kisinda dakika ya nne, Yacouba Songne dakika ya saba na Michael Sarpong aliyefungwa kwa penalti dakika ya 28 huku goli la Africal Lyon likifungwa na Mwarami Abdallah.
Baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliochezewa kwenye uwanja wa Azam Complex, kocha Kaze alisema kuwa, Carlinhos ni mchezaji mzuri aliyempa chaguo lingine na yupo vizuri kiufundi uwanjani hata katika kutoa pasi.
Amesema, mchezaji huyo ana uwezo wa kuona nafasi uwanjani lakini kwa sasa tunajenga utimamu wake ili awe vizuri kwenye kutoa ushindani na kuhimili mikiki mikiki ya dakika 90.
Hata hivyo akizungumzia kiwango cha wachezaji wake katika mchezo huo, Kaze amesema kuwa, wachezaji wake wameanza kumuonesha kile alichokuwa akikihitaji kwani dakika 20 za mwazo waliweza kufanya vizuri huku pia akivutiwa na maamuzi waliyokuwa wakiyafanya
Katika kipindi cha pili bado wachezaji wake walicheza vizuri lakini haikuwa kama kipindi cha kwanza lakini jambo kubwa wanashukuru kuona mapungufu hayo ambayo wanahitaji kuyafanyia kazi kabla ya mchezo wao ujao dhidi ya Namungo.
Amesema kuwa, kazi kubwa aliyonayo sasa ni kufanyia kazi makosa aliyoyaona kwenye mchezo huo hasa katika safu yao ya ushambuliaji ambayo licha ya kutengeneza nafasi nyingi za mabao lakini walishindwa kuzitumia ipasavyo.
Licha ya kujitahidi lakini kocha huyo amesema, washambuliaji wanatakiwa kujua eneo hasa wanalotakiwa kuwepo na ameona katika mchezo huo walikuwa wanaachia sana safu ya ulinzi ya wapinzani wao kuanza mpira na kucheza uvivu hivyo wanahitaji zaidi kuweka presha kwa mabeki wa wapinzani wao.
“Tunaamini mechi hii ya kirafiki itawajengea zaidi wachezaji wetu kujiamini, kujenga muunganiko mzuri lakini pia imetupa nafasi ya kuona mapungufu yetu kabla ya mchezo wa Ligi dhidi ya wapinzani wetu Namungo FC,” amesema Kaze.
Amesema kuwa, anatarajia katika maandalizi ya mchezo huo, wachezaji wao am bao kwa sasa wapo katika majukumu ya timu ya Taifa watakuwa wamesharejea ili kumpa nafasi ya kuangalia ni namna gani watazipata alama tatu katika mchezo huo ujao.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025