Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
WAKATI kocha mpya wa klabu ya Yanga, Cedric Kaze akiendelea kusuka upya kikosi chake ili kuhakikisha kinakuwa moto wa kuotea mbali katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) tayari vigogo wa klabu hiyo wameshaanza kumpa siri za wapinzani wao ambao walionekana kuwapa wakati mgumu msimu uliopita.
Kocha huyo amejiunga rasmi na klabu hiyo mwishoni mwa wiki baada ya kusaini kandarasi ya miaka miwili akirithi mikoba ya Mserbia Zlatko Krmpotic ambaye alitimuliwa licha ya kuipa timu hiyo ushindi wa kwanza mnono wa goli 3-0 katika mchezo dhidi ya Coastal Union.
Kelele za mashabiki wengi wa klabu hiyo ilikuwa ni kuona timu yao inapata ushindi wa zaidi ya goli mbili baada ya kufunga goli moja katika mechi zao za awali za msimu huu mpya.
Ujio wa Kaze ambaye anaichukua timu hiyo inayoshika nafasi ya tatu wakiwa na alama 13 walizopata baada ya kushinda mechi nne na sare moja ni faraja kubwa ya mashabiki wa Yanga ambao wanatarajio timu yao kupata ushindo mnono katika mchezo wao ujao wa Ligi Kuu.
Kibarua cha kwanza cha kocha huyo kitakuwa Oktoba 22 katika mchezo namba 53 wa Ligi Kuu dhidi ya Maafande wa Polisi Tanzania utakaochezwa saa 1:00 usiku katika uwanja wa Mkapa.
Kuelekea kwenye mchezo huo, tayari viongozi mbalimbali wa klabu hiyo wameanza kumpa siri za wapinzani wao hao pamoja na wengine am bao watakutana nao siku chache zijazo ikiwemo mahasimu wao Simba watakaomenyana nao Novemba 7.
Mchezo huo pia unatajwa huenda ukavunja rekodi ya mashabiki wa Yanga msimu huu kwani wengi wamepania kushuhudia ubora wa kikosi chao katika mchezo wa kwanza ambao Kaze atakuwa kiongoza benchi la ufundi la klabu hiyo.
Jambo lina linatajwa kuchagizwa na ahadi aliyotoa kocha huyo mara baada ya kutua hapa nchini akidai atahakikisha idadi ya mashabiki inaongezeka kutokana na soka safi na la kisasa litakalooneshwa na wachezaji wake.
Kupitia mtandao rasmi wa klabu hiyo, kocha wa zamani wa klabu hiyo, Kenny Mwaisabula ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ameweka wazi kuwa, watahakikisha wanampa kila aina ya ushirikiano kocha huyo ambaye pia ameshawaonesha anahitaji ushirikiano nao kwani wanalijua zaidi soka la hapa nchini.
Amesema, watamfatilia kwa karibu kuanzia katika mazoezi na kumpa mbinu za nini anapaswa kufanya ili kuhakikisha timu yao inapata ushindi katika kila mchezo ulio mbele yao.
“Kwa ajili ya mafanikio ya timu yetu tutajitoa kwa kila namna ili kuhakikisha tunampa kila mbinu za wapinzani wetu kocha wetu mpya ambazo zitampa ushindi, lakini pia anatakiwa kuwa huru kutuuliza jambo lolote ikiwemo kuhusu wachezaji. Tunatambua kuwa yeye ni muamuzi wa mwisho lakini kwa nafasi yetu tutampa ushauri kwani taaluma ya ukocha kila mtu anajua kilicho bora,” amesema Mwaisabula.
Lakini pia amewataka mashabiki kupunguza mihemko na kumpa muda kocha huyo ambaye ndio kwanza ameichukua timu ambayo ilikuwa na mapungufu kadhaa ikiwemo kutokuwa na muunganiko mzuri.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania