Na Mutta Robert,TimesMajira Online,Geita
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) umeanza zoezi la kuhakiki kaya zote maskini katika Mkoa wa Geita ambazo zinanufaika na fedha za mfuko huo ili kubaini kaya hewa na kuziondoa katika orodha ya malipo.
Akizungumza na katika mafunzo kwa wawezeshaji ngazi ya Halmashauri Afisa Mradi wa TASAF kutoka Makao Makuu, Mary Mtambalike amesema kuwa, zoezi la uhakiki linafanyika katika mkoa mzima wa Geita kwa muda wa siku tatu mfululizo baada ya kumaliza mafunzo hayo ya siku mbili.
Amesema kuwa, zoezi hilo linafanyika baada ya agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kuagiza kaya zote ambazo hazina sifa ya kuwa maskini kuondolewa kwenye malipo na kulipa watu wanaostahili na wana sifa za kuwa maskini.
Mtambalike ameongeza kuwa,zoezi hilo litafanyika kwa njia ya kielektroniki ambapo wawezeshaji wa kufanya zoezi hilo watatumia vifaa vya kisasa kujaza taarifa za wanufaika kwa kutumia Kishikwambi (Tablet) kwa kuongozwa na maswali ya dodoso ambalo limeandaliwa.
Zoezi hilo linafanyika katika wilaya zote za Mkoa wa Geita ikiwa ni kuondoa watu ambao hawana tena sifa kama kaya za viongozi,watu wenye uwezo wa kiuchumi au ambao walishafariki .
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Modest Apolinary akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, amesema, kaya zote ambazo hazina vigezo vya kuwa masikini au wale ambao walishaondoka kwenye kundi la maskini lazima waondolewe wote kwenye orodha ya wanufaika.
Christina Chitanda mwezeshaji ngazi ya halmashauri ambaye ameshiriki mafunzo hayo kwa ajili ya kwenda kushiriki kuakiki kaya hizo amesema, amepata mafunzo yatakayomuwezesha kubaini kwa kutambua kaya zenye sifa za kuendelea kuwa kwenye orodha ya kaya maskini na ambazo zina sifa za kuondolewa.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi