November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaya 78,414 kupatiwa vyandarua

Na Lubango Mleka, Timesmajira Online,Igunga.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora imezindua rasmi zoezi la ugawaji wa vyandarua vya kujikinga na malaria vipatavyo 311,324 kwenye vituo 726 ambapo takribani kaya 78,414 zinatarajiwa kugaiwa vyandarua hivyo.

Hayo ameyabainisha Novemba 3,2023 na Kaimu Meneja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Tabora Adonizedeck Tefurukwa ambaye aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Mkuu wa wao ambapo amesema MSD ndiyo msambazaji mkuu wa bidhaa za afya kwenda kwenye vituo zaidi ya 7,000 vya Umma na vile vya binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya.

Kaimu Meneja wa MSD kanda ya Tabora Adonizedeck Tefurukwa

Amebainisha kuwa ili kurahisisha zoezi la usambazaji wa vyandarua hivyo ambavyo kaya hizo zinatarajia kunufaika MSD imekodi ghala moja wilayani hapo ili kurahisisha zoezi la kusambaza vyandarua hivyo kutoka katika ghala hilo mpaka kwenye vituo vya kupokelea.

“Bohari ya Dawa tunayo miundombinu wezeshi na uzoefu wa kutosha, hivyo tunatarajia gharama za usambazaji kuwa rafiki zaidi pia kurahisisha upatikanaji wa takwimu katika bidhaa za afya umeongezeka na gharama za bidhaa hazijapanda, kwa muktadha huu tupo tayari kusambaza vyandarua hivi ndani ya Halmashauri ya Igunga,” amesema.

Pia amewaasa wananchi wa Igunga kwenda katika vituo walivyojiandikisha ili kupatiwa vyandarua huku akizitaja faida za kutumia vyema vyandarua ni kwa ajili ya kujikinga na mbu waenezao ugonjwa wa malaria,kupunguza gharama za matibabu na kuongeza pato la familia kwa kuwa na nguvu kazi yenye afya njema.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Ofisa Elimu Sekondari Benjamin Siperito ameishukuru serikali kwa uzinduzi wa zoezi hilo katika Halmashauri hiyo jambo ambalo linakwenda kukinga na kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwani mvua za masika zimeanza jambo linalopelekea kuwepo kwa mazaria ya mbu waenezao malaria.

Katibu Tawala Wilaya ya Igunga Elizabeth Rewegasira (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wilaya ya Igunga, viongozi wa MSD na baadhi ya wananchi waliojitokeza kupatiwa vyandarua Novemba 3,2023 katika uzinduzi ulifanyika enoo la Soko la Kati Igunga Mjini

Naye, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga Lucia Kafumu ameeleza kuwa wilaya hiyo imepunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria kutoka asilimia 15 na kufikia asilimia 5.6 na kuwataka wananchi kuzingatia kanuni za afya na miongozo ya kujikinga na magonjwa ambukizi yatokanayo na uchafu kwani imebainika hospitali ya wilaya ya Igunga inapokea wagonjwa wengi hasa watoto wenye magonjwa ya kuhara.

Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Elizabeth Rewegasira amesema kuwa, wilaya kupitia serikali kuu imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa wa Malaria, uhamasishaji wa usafi wa mazingira ili kuangamiza mazaria ya mbu.

“Mazingira ya mji wetu ni machafu sana hivyo ninawaomba kila mmoja wetu kwenye nyumba zetu kwa kushirikiana na watendaji,viongozi wa mtaa na Serikali kuhakikisha kila nyumba imefanya usafi wa mazingira kwa kufukia madimbwi yote kwani mvua inakuja na itaweka maji katika madimbwi ambayo ni mazaria ya mbu waenezao malaria,” amesema Rewegasira.

Amewataka wananchi hao kwenda kuvitumia vyandarua hivyo kwa matumizi ya kujikinga na mbu waenezao ugonjwa wa malaria na si vinginevyo kwani ibainika kuwa wamevitumia kufugia kuku, kutunzia bustani na kuvulia samaki, atachukukuwa sheria kwani ni kinyume na malengo ya serikali.

Viongozi wakifuatilia burudani mbalimbali katika uzinduzi wa zoezi la ugawaji vyandarua katika uwanja wa Soko la Kati Igunga Mjini

Pia amewataka wananchi kuacha kusikiliza maneno ya upotoshaji juu ya zoezi la ugawaji wa vyandarua ikiwa ni pamoja imani ya kuishiwa nguvu za kiume kwani jambo hili sio la kweli, hivyo lengo la ugawaji wa vyandarua hivi ni kujikinga na malarai na kuhakikisha wilaya inafikia asilimia 0 ya maambukizi ya ugonjwa wa malarai.

Just Doto ni moja ya wananchi aliyepatiwa vyandarua amesema kuwa anakwenda kuvitumia vyandarua hivyo kama ilivyo elekezwa na atakuwa balozi mzuri katika kutoa elimu waliyopatiwa juu ya matumizi ya vyandarua.