Judith Ferdinand na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
Mbunge wa Jimbo la Ilemela,Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula,amesema suala la uwekezaji bandari ni ufunguo wa uchumi wa Taifa hili.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza kwa niaba ya Wabunge wa Kanda ya Ziwa katika mkutano wa hadhara wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa uliofanyika uwanja wa CCM Kirumba wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
“Suala la uwekezaji wa bandari ni ufunguo wa taifa letu kiuchumi,wale ambao hawajelewa tutasubiri ufahamu wao ufunguke,”ameeleza Dkt.Angeline.
Sanjari na hayo amefafanua kuwa Sheria ya Ardhi Namba 4 inabainisha namna bora ya kumilikisha ardhi kwa wawekezaji,watapewa hati ya muda wa kupanga katika ardhi hiyo si kuwamilikisha jumla.
Pia amesema chini ya uongozi wa Rais Samia,shughuli za maendeleo hazijasimama mkoani Mwanza na Jimbo la Ilemela ambapo Tirioni 4.556 zimetolewa kwa miradi ya kimkakati na kuimarisha huduma za jamii.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi-Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema,bandari ndio malango yanayoingiza shehena kubwa ya mizigo nchini hivyo bandari inayotegemewa nchini ni ya Dar es Salaam ambayo ikiboreshwa bandari zote zitakuwa bora.
Pia aliitoa ufafanuzi kwa wananchi kuwa bandari ya Dar-es-Saalam itapangishwa magati matano na siyo kuuzwa kama inavyodaiwa na wapotoshaji ambapo bandari za Ukerewe, Mwanza Kusini na Kaskazini,Kemondo na Bukoba ikiwemo ya Muharamba zitaendelea kuwepo.
Amesema mwaka wa fedha ulioisha mapato ya bandari zote nchini yanayosimamia na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) yalikuwa bilioni 795.2 na kutumia zaidi ya bilioni 791 huku TRA ikikusanya trilioni 7.76 katika bandari ya Dar es Saalam, hivyo upitia uboreshajina uwekezaji wa bandari makusanyo ya TRA yataongezeka mpaka trilioni 26.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni,Wakili Albert Msando amesema Oktoba 25, 2022 serikali iliingia mkataba wa makubaliano ya kuendeleza, kusimamia na kuendesha shughuli za bandari mkataba ambao baada ya kusainiwa uliridhiwa na Bunge.
“TPA haijauza bandari na hakuna mwekezaji ameuziwa ardhi ya bandari, masuala yote ya ardhi yatasimamaiwa kwa mujibu wa sheria halali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Sheria namba 4 ya Ardhi imeweka wazi, waache uongo hakuna bandari imeuzwa,”amesema Wakili Msando.
Naye Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula,amesema kwa bajeti ya trilioni 44.3, bado taifa linahitaji kupata vyanzo vingi vya mapato hili bajeti hiyo ilifikie asilimia 100 na kuwezesha miradi ya kijamii itekelezwe kwa ufanisi hivyo uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam unahitajika.
Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Ezra Chiwelesa amesema wapo kwetu majimbo kuzungumza na wananchi kuhusu miradi iliyotekelezwa na serikali kwani Rais ameiheshimisha nchi kwa miradi ya elimu na maji.
“Sisi wabunge wa Kanda ya Ziwa tunaunga mkono mpango wa kuwekeza katika bandari ya Dar es Saalam,jambo hilo liharakishwe ili kuinua uchumi wa wananchi,mapato na kuongeza ajira,”.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla,kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa ya Kanda ya amemshukuru Rais Samia kuleta fedha katika Mkoa huo kiasi cha trilioni 1.4 za miradi ya maendeleo ikiwemo ya kimkakati huku akiridhia kutoa bilioni 130 za kuiwezesha Wilaya ya Ukerewe kupata umeme wa uhakika.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni Daraja la Kigongo-Busisi ambao umefikia asilimia zaidi ya 75,SGR kipande cha Mwanza-Isaka kinachojengwa kwa trilioni 3 umefikia asilimia 32,Meli ya MV Mwanza iliyogharimu bilioni 108 umefikia asilimia 95 huku ukarabati wa meli ya mizigo ya MV.Umoja ukigharimu bilioni 20.
“Yanayoendelea ya uwekezaji wa bandari ni wivu wa maendeleo na siasa ambapo siasa hujibiwa kwa siasa,uongo ukiachwa unakuwa ukweli,hivyo wananchi wa Kanda ya Ziwa wanaunga mkono uwekezaji huo kwani watakuwa wanufaika wakubwa kupitia bandari Kavu Fella,meli ya Umoja na daraja la Kigongo-Busisi, zitapokea mizigo na kuisafirisha kwenda nchi jirani,”.
CCM kupitia Katibu Mkuu wake Daniel Chongolo wamehitimisha mkutano wa hadhara maalumu kwa ajili ya kuelimisha wananchi kuhusu mkataba wa uwekezaji na uendelezaji wa bandari katika Mkoa wa Mwanza baada ya kufanya mikutano mingine 7 ikiwemo Mbeya, Mtwara,Arusha,Tanga,Singinda, Kigoma,Dar-es-Salaam.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini