January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kauli ya Kinana imedhihirisha sura mbili za viongozi CHADEMA

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Dar

KWA muda mrefu Watanzania wamekuwa wakisikiliza kauli za upande mmoja kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusiana na vikao vya maridhiano baina yake na Serikali ya CCM.

Kuzaliwa kwa vikao vya maridhiano hayo ilikuwa ni matokeo utashi wa Rais Samia na mazungumzo yake na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

Mara baada ya Mbowe kufutiwa kesi ya ugaidi na kuachiwa huru kutoka kwenye kuta nne za Gereza la Ukonga, Mbowe aliitwa Ikulu na Rais Samia na kufanya mazungumzo.

Mara baada ya mazungumzo yao waliongea na waandishi wa habari na wote walichokisisitiza ni haki kwenye kila jambo. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa kuanza kwa vikao vya maridhiano ambavyo vilikuwa siri.

Hata hivyo, baadaye CHADEMA ilitangaza kuwa Serikali ya CCM haina dhamira ya dhati ya kuleta maridhiano, lakini haikueleza mazuri ambayo imenufaika nayo.

Aidha, chama hicho kimeitisha maandamano ambayo kinadai hayana ukomo kushinikiza kuondolewa au kutosainiwa na Rais Samia miswaada ya sheria ya uchaguzi kuwa sheria.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye kongamano la Baraza la Wanawake wa CJHADEMA (BAWACHA) lililofanyika mkoani Kilimanjaro. Moja ya sababu zilizomsukuma Rais Samia kuhudhuria mkutano huo ni matokeo ya vikao vya maridhino baina ya CHADEMA na Serikali ya CCM.

Aidha, chama hicho kimekuwa kikidai kuwa vikao vya maridhiano ambavyo vimekuwa vikifanyika zimekuwa zikipigwa picha ambazo Serikali ya CCM inazitumia kuonesha Ulimwengu kwamba nchini kuna naridhiano baina ya chama hicho kikuu cha upinzania na Serikali ya CCM.

***Je ni kikweli vikao vya maridhiano havijazaa matunda

Kitendawili hiki kimeteguliwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdurahaman Kinana, akianza kwa kuvishauri vyama vya siasa vya upinzani hususan CHADEMA, kuacha kufanya maandamano yasiyo na msingi badala yake wathamini nia njema aliyonayo Rais Dk. Samia katika kuleta maridhiano na kuwatumikia Watanzania.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kufafanua kwa kina ubora wa miswaada ya uchaguzi ambayo imepitishwa na Bunge hivi karibuni, baada ya wadau mbalimbali nchini kutoa maoni yao ambapo amesisitiza sheria hiyo itakuwa bora kuliko iliyopo sasa.

Kinana aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam alipozungumza na wana CCM na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, ambapo mbali ya kutumia muda mwingi kuzungumzia, maridhiano yaliyoingiwa kati ya CCM na CHADEMA pamoja vyama vingine vya upinzani, anasema kuna mambo mengi mazuri yamefanyika.

Anasisitiza kuwa kuna mambo mazuri yamefanikisha kupitia vikao vya maridhiano.

***CHADEMA yapata ruzuku ya bilioni 2.7/-

Kinana anasema CHADEMA haitaki kueleza ukweli ikiwemo Serikali kukipatia chama hicho ruzuku ya Sh.bilioni 2.7 ambayo waliikataa kwa miaka mitatu nyuma.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akizungumza na Rais Samia Suluhu Hassan, mara baada ya kufutiwa kesi ya ugaidi.

Chama hicho kilikataa ruzuku hiyo kikipinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020, huku kikiweka wazi kwamba hakiwezi kupokea ‘mazao’ yaliyotokana na uchaguzi huo.

Aidha, Chama hicho kiliwafuta wanachama wake 19 ambao ni wabunge wa viti maalum, lakini kwa kupitia mlango wa nyuma kimepokea ruzuku ya sh. bilioni 2.7 ambayo inatokana na wabunge wake wanaoitwa COVID 19.

***Miswaada ya sheria za uchaguzi

Akielezea kuhusu miswaada ya sheria za utaguzi, Kinana anasema pamoja na uzuri wake ikiwemo kuzingatia maoni ya wadau wakiwemo CHADEMA wenyewe, lakini bado kinasema haifai.

“Nilifikiri sheria hii mpya wangesema itatufikisha mbali zaidi, lakini wao wanasema hii haifai, basi turudi kule. Sheria ya sasa ni bora kwa muundo, kwa maudhui, kwa malengo, kwa dhamira sijui mnanielewa?

Nitumie nafasi hii kuwasihi ndugu zangu wa CHADEMA waungane na Watanzania waachane na mandamano, waangalie dhamira ya Rais.

“Hivi Rais na baraza lake la mawaziri kama wasingepeleka hii sheria mpya ya uchaguzi nani angemlazimisha?

***Busara imemuongoza Rais Samia

Kinana anasema busara imemuongoza akasema hapana hebu twende pamoja na mimi ndio mtetezi mkubwa wa maridhiano na ustahimilivu. Hebu tupeleke sheria mpya bungeni na kila hoja aliyopelekewa, aliyoambiwa kwamba haya ndio maoni ya wadau Rais akasema sawa, nakubali.

“Sasa niwasihi ndugu zangu Watanzania, tujipange kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa, tujipange kwa uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Sheria hii ni nzuri, bora kuliko sheria yoyote iliyopo katika historia ya nchi yetu, inakidhi mahitaji na matakwa ya nchi na jumuiya ya madola, inakidhi mahitaji ya nchi za Umoja wa Afrika (AU), inakidhi vile vile mahitaji ya nchi za Kusini mwa Afrika ambao na sisi ni wanachama,” alisema.

Aliongeza kwamba hakuna tume ya miujiza zaidi itakayokuwepo, huku akifafanua kila jambo ambalo litafanyika lazima litakuwa na kasoro moja au mbili, na kuhoji kwani CHADEMA wao hawana kasoro?.

“Wanazo, sasa nawaambia ninyi chama kikuu cha upinzani kuweni basi na ustahimilivu kidogo, uungwana na kusikiliza wenzenu na kuona nia njema iliyopo katika Chama Cha Mapinduzi, kwa na serikali yake,” alisema.

Akifafanua zaidi Kinana alisema kuwa kushinda uchaguzi kunatokana na sera, mipango ya uchaguzi na kusikiliza watu, kwani unaweza kuwa na tume nzuri ya uchaguzi na matokeo yakawa ni ya hovyo, usiyoyataka.

Alitoa mfano wa moja ya nchi jirani ambayo walipigania sana kuwa na tume huru kwa miaka 20, wakaipata, lakini wamegombea mara nne hawakupata.

“Hawakuingia madarakani, wale waliotengeneza hiyo tume hawakupata, sasa wanasema Katiba hii haina maana waifute, wale walioingizwa na katiba baadae nao wakashindwa wanasema katiba hii haina maana.

Kwa hiyo aliyeshinda anasema Katiba haina maana na aliyeshindwa naye anasema Katiba haina maana.

“Sasa kushinda uchaguzi sio Katiba tu, Nigeria baada ya wanajeshi kutoka baradakani walitengeneza Katiba mpya mwaka 1969 na kwa sehemu kubwa walienda kuchukua Katiba ya Marekani, tume ya uchaguzi ya Rais inateuliwa na Rais kwa kushauriana na baraza la ushauri.

“Baraza la ushauri ni nani? Rais ndio Mwenyekiti, makamu mwenyekiti ni makamu wa rais, wajumbe wengine marais wastaafu, hapo vipi? Kuna mtu anatoka nje ya mfumo?

“Hao ndio wanateua, mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa tume, uchaguzi unafanyika na watu wanakubali. Hapa tunatafuta malaika wa kuja kuongoza tume, kila utakachofanya unaambiwa kinakasoro, hivi mnavyoona yote tuliyokubali wanasema hamna kitu.

***Maandamano

“Nimesikia wanaandaa maandamano Mwanza, Mbeya na Arusha na mimi nataka niwasaidie kutangaza kama watu wengine hamjasikia. Wanakwenda kueleza haya yaliyopitishwa na CCM na Bungeni hamna kitu.

“Tume si kila kitu, Namibia kamati inatengenezwa baada ya pale anayetua Rais, kuna nchi inaitwa Mauritius na hizi nchi zote ambazo nimezitaja ni za Jumuiya ya Madola, Rais anashauriana na watu wawili tu, anashauriana na waziri mkuu na kiongozi wa upinzani bungeni hakuna mtu mwingine,” alisisitiza.

“India wana mkurugenzi na wana makamishina. Nani anateua? Waziri Mkuu na Baraza lake la Mawaziri kwisha, yaani Rais Samia akae na baraza lake la mawaziri atengeneze orodha ateue, si moto utawaka hapa? Watasema tu maigizo.

“Sasa kuna shida hapa nchini kila unalofanya halina heri ndani yake, lakini vizuri haya mambo tukayaeleza maoni mengine yakatolewa unajua siku hizi kuna watu wanapita bila kupingwa lakini ni vizuri wanaopita bila kupingwa wakapigiwa kura ya ndio au hapana Bunge likasema sawa tumekubali.

“Wanauliza kwa nini? Wanasema kuna watu wengine wanafanya ujanjaujanja wa kupita bila kupingwa, hivyo wapigiwe kura tujue kama wanakubalika Bunge limesema sawa itapigwa kura ya ndio au hapana,” alisema.

*** Matunda ya maridhiano, kesi nyingi zafutwa

Akizungumzia maridhiano ambayo yamefanyika kwa nyakati tofauti, Kinana anasema kuwa wakati Rais Samia anaingia madarakani kulikuwa na wanachama wa CHADEMA wasiopungua 400 wako mahabusu wakikabiliwa na kesi zilizotokana na sababu mbalimbali za kiuchaguzi, lakini ulitengenezwa utaratibu wa kisheria waakachiwa huru.

Kinana anasema hakuna maridhiano bila ustahimilivu, Rais alialika taasisi za kidini na kiraia ili waelewane kujiuliza nini wanahitaji kwa lengo la kuhakikisha tunakuwa na taifa liwe la watu wenye mshikamano na kupendana.

Alisema Dkt. Samia aliunda tume ya kusikiliza makundi ya Watanzania kusikiliza hoja zao ikiwemo Katiba, lakini mwishowe CHADEMA waligomea kwa sababu zao.

***Kauli ya Kinana yaibua wadau

Kauli ya Kinana kuweka wazi ‘ukigeugeu’ wa CHADEMA imezidi kuwaibua wadau wa siasa nchi nchini wakiwemo wasomi ambo wamekitaka chama hicho kuwaomba radhi wananchi.

Wasomi na wachambuzi, wameshangaa kitendo cha CHADEMA kuendelea kuhamasisha maandamano na kukosoa baadhi mambo, huku wakiacha kusema ukweli kwamba maridhiano ha hayo hayo yamewawezesha kupata ruzuku ya sh. bilioni 2.7 ambayo waliigomea kwa zaidi ya miaka mitatu.

Mwanasiasa mwenye historia kubwa ya siasa na uongozi nchini, Hamad Rashid Mohamed, aliipongeza CCM kwa miaka 47 ya kuzaliwa kwake chini ya Mwenyekiti wake Rais Dk. Samia ambaye ametembea ipasavyo mkakati wake wa 4R.

Anasema hatua ya Rais Dkt. Samia kusimamia maridhiano na Bunge kupitisha miswada mitatu ukiwemo wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria wa Marekebisho ya Vyama vya Siasa yote ikiwa ya mwaka 2023 ni ya kupongezwa.

“Binafsi nimshukuru sana Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara mzee wetu Kinana kwa kweka wazi hili na huenda kuna mengi ya siri hatuyajui, hii ni aibu kwa viongozi wakuu wa chama hicho.

“Hii ni aibu na fedheha kwa Chama kikubwa cha upinzani kama CHADEMA kuwa na kauli mbili mbili, kauli za hadharani na sirini, huku kwa wananchi wakiwa wanajipambanua kuwa wao ni chama cha ukweli na uwazi. Wamekuwa watu wa kuhimiza maandamano lengo lao ni kutafuta huruma za wananchi huku wakiwa wanapita mlango wa nyuma na kujichumia fedha kimya kimya,” anasisitiza.

Anasema kama kweli Chama hicho ni cha uwazi na uwajibikaji wakiri makosa yao na kuomba radhi kwa kuwa fedha hizo za ruzuku walizisusa kwa zaidi ya miaka mitatu wakiwa wametangaza hadharani, hivyo hatua ya viongozi kurudi kimya kimya na kuzichukua si jambo jema.

“Pia tutoe rai kwa hawa wenzetu waache kukitumia Kikosi kazi cha maridhiano vibaya na kujichumia matumbo yao, hawa watu wanachuma ndani ya serikali na wanachuma nje ya nchi kwa madai ya kuomba msaada katika kuimarisha demokrasia, hiki ndio kisebusebu sasa,” alisema.

Anasema jambo hilo la kupokea zaidi ya sh. bilioni 2.7 lingekuwa jema kwao wasingefanya siri bali wangetangaza kama ambavyo wamekuwa wakitangaza mengine.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha ADC Doyo Doyo, alisema maridhiano yaliyonzishwa na Rais Dk. Samia yameleta umoja katika vyama vya upinzani.

Doyo anasema awali ilikuwa huwezi kukaa ukumbi mmoja na wanachama wa CCM, lakini maridhiano yaliyoletwa na Rais Dk. Samia yameleta umoja kwa wanansiasa.

“Mariadhiano ya kweli yanajenga siasa ya Tanzania na kukuza demokrasia nchini,”anasema

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Dkt. Thimothy Lyanga, anasema Kinana ametoa ufafanuzi namna serikali ilivyofanikisha hatua ya maridhiano, huku akihimiza siasa za kistaarabu.

Anasema kutokana na kauli ya Kinana ni wazi CHADEMA wamefedheheka hivyo ni vyema kurudi na kuwa waungwana kwa kuuthibitishia umma kuwa ni kweli Rais Dkt. Samia alikuwa mstaarabu na kuridhia wao kupata stahiki hizo za ruzuku.

“Uungwa ni CHADEMA kurudi na kuthibitisha katika uwanja wa siasa kuwa jambo hili ni kweli, uungwana unazaa amani na utulivu na wanatambua kuwa siasa zao zinachochea uvunjifu wa amani.

“Hiki ni chama kikubwa cha siasa wasipokuwa wakweli wawazi wanaendelea kupoteza sifa na heshima ambayo wananchi wanawapatia fedha hizi ni za umma wamechukua waseme,”anasema.

Anasema, hatua ya Rais kudhamiria kuwapo kwa maridhiano na kuongoza nchi kwa hekima na uvumilivu imelenga kuwapa nafasi wananchi ya kumchagua wamtakaye hivyo isitafsiriwe tofauti na vyama vya siasa kwa kulazimisha kuwapo na uongozi wa mabavu.

“CHADEMA wajitafakari wananchi wameamka wanaona miradi inayotekelezwa na wanaona namna Rais alivyojipambanua kuwa na siasa za kistaarabu wasilazimishe vurugu,”alisema.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT) Dkt. Mohamed Maguo anasema maridhiano ya kweli ndio yanayosababisha nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu.

Dkt. Maguo anasema Rais Dk. Samia amekuwa kiongozi wa mfano wa kulitaka taifa lisijigawe na ndio maana alizianzisha 4R kwa lengo la kutaka maridhiano ya kweli akianzia kwa wanasiasa.

“Nchi haiwezi kuwa na amani, utulivu,umoja na maendeleo bila ya kuwepo kwa maridhiano ya kweli na ndio maana tayari Rais Samia alishakaa meza moja na Mwenyekiti wa CHADEMA ili kutafuta suluhu ya kweli,”alisema Dkt. Maguo.

Dkt. Maguo anasema Taifa linashuhudia miaka 47 ya CCM ambayo yameleta tija nchini.

Anasema tija hiyo imetokana na wananchama wa chama hicho kuwa na maridhiano ya kweli ikiwemo kusikilizana na kushauriana .

“Masikilizano ya wanasiasa ni ukomavu wa kidemokrasia na kuhifanya nchi husika kuendelea kupata maendeleo kwa sababu ya ushirikiano uliopo,”alisema .

Kwa upande wa mchambuzi wa masuala ya siasa nchini ambaye ni Mhadhiri wa Chuo cha Mwalimu Nyerere Dkt. Philip Daninga, anasema Rais Dkt.Samia ana nia njema na watanzania na ndio sabbau ya kufanyia kazi yale ambayo yaliyokuwa yanaleta ugumu kwa wapinzani.

Alisema Rais Dkt. Samia alitumia 4R kwa kuruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama vya upinzani kwa lengo la kuleta haki katika vyama hivyo na si unyonge.

Pia alisema miaka 47 ya CCM Chama hicho kimeweza kupiga hatua hasa katika kutunza amani na utulivu vilivyopo nchini.

“Maridhiano ya kweli yanaleta amani ya kweli katika nchi na ndio maana Rais Dk. Samia tangu aingie madarakani anatafuta maridhiano ya kweli na vyama vya upinzani ili Taifa liongee lugha moja,”anasema

Anasema Rais Dkt. Samia katika miaka mitatu yake ya uongozi ameweza kuitangaza vyema nchi na kusababisha kuwepo kwa mahusiano mazuri kati ya nchi na nchi.

“Naipongeza CCM kwa sababu mambo mazuri mengi tunayoyaona hasa yale mazuri yameletwa na CCM kwa sababu historia ya Tanzania haiwezi kukamilika bila ya kutaja chama hicho.