Na Ashura Jumapili ,TimesMajira online Geita
Serikali imesema itaupatia Mji Mdogo wa Katoro Mkoa wa Geita Wilaya ya Kipolisi na kuujengea kituo kipya cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya ili kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa Mkoani Geita.
Naibu Waziri Sillo, amesema sababu za kupeleka hitaji hilo, ni kutokana na Mji wa Katoro wenye watu zaidi ya laki tatu kukua kibiashara na kiuchumi kwa kasi.
“Kituo cha Polisi kilichopo kipo katikati ya makazi ya watu na maeneo ya biashara habari njema ni kwamba IGP alituma timu yake hapa walishafanya tathimini.Hivyo mnajengewa kituo kipya cha kisasa na mnapatiwa Wilaya ya Kipolisi hapa Katoro,”amesema Sillo.
Pia amewahimiza Polisi Kata nchini kuendelea kutoa elimu ya polisi jamii kwa wananchi na viongozi wa Serikali za mitaa, kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ili kupambana na kutokomeza uhalifu, unaojitokeza maeneo mbalimbali ikiwemo wizi wa mifugo unaotajwa kuwepo kwa wingi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
“Wananchi mnapata taarifa za wezi, mnakaa nazo na wengine kuishi nao naomba toeni taarifa kwa Jeshi la Polisi ili sheria ichukue mkondo wake,”amesema Sillo.
More Stories
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa