January 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu Dkt. Jingu: Safari Chanel kuitangaza nchi yetu

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu ameeleza kuwa uwepo wa safari chaneli ni fursa ya kipekee kuendelea kuitangaza nchi yetu ndani na nje na kuchagiza ukuaji wa uchumi.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara wadau wa Tanzania Safari Channel (TSC) kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Mei 30, 2022 Jijini Dodoma.

“Safari chaneli ni moja ya nyenzo ya kukuza utalii wetu na sisi kama wadau tuna jukumu la kuhakikisha tunawekeza vya kutosha katika maeneo muhimu ikiwemo rasilimali fedha zitakazosaidia kuendesha chaneli hii ili malengo ya uwepo wake yatimie,”alisisitiza Dkt. Jingu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi alieleza kuwa uwepo wa chaneli hiyo utasaidia katika kuvutia na kuongeza hamasa kwa watalii kuingia nchini.

“Tanzania Safari Channel ni msaada katika kuutangaza utalii, na kuitangaza nchi yetu na hii ni fursa kwetu nitoe wito kwa taasisi mbalimbali kuendelea kutangaza na kuitumia fursa hii ili kuendelea kukuza uchumi wetu,”alieleza Dkt. Yonazi

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Fatma Hamad Rajab alipongeza hatua ya uwepo wa chaneli ya hii, huku akieleza jitihada za Zanzibar kuanzisha chaneli ya utalii itakayosaidia kuitangaza na kuonesha vivutio vilivyopo.

“Kwa upande wa Zanzibar tuna mpango wa kuwa na chaneli ya ZBC 3 inayolenga kuonesha masuala ya utalii hatua hii inadhihirisha namna viongozi wetu kwa pande zote mbili wanavyojitahidi kutangaza vivutio vyetu vya utalii tunaahidi kuendelea kuwaunga mkono kwa kuhakikisha tunakuwa wabunifu katika kutangaza utalii wetu,”alisema Fatma.

Alihitimisha kuwa chaneli hizi zitasaidia kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu tamaduni zetu hivyo kudumisha.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Dkt. John Jingu akiongoza kikao kazi cha Makatibu Wakuu wa Wiazra wadau wa Tanzania Safari Channel (TSC) walipokutana katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 30 Mei, 2022.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi akichangia jambo wakati wa kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara wadau wa Tanzania Safari Channel (TSC) Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Kaspar Mmuya akifafanua jambo wakati wa kikao hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayubu Ryoba akizungumza wakati wa kikao kazi cha Makatibu Wakuu wa Wizara wadau wa Tanzania Safari Channel (TSC) Jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara wadau wa Tanzania Safari Channel (TSC) wakifuatilia kikao hicho