February 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katavi yazindua mkakati wa kupambana na udumavu

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.

MKOA wa Katavi umezindua rasmi mkakati wa kupambana na udumavu unaosababishwa na utapiamlo kwa kuhakikisha suala la lishe duni linatokomezwa kwa wananchi.

Hatua hiyo inakuja baada ya viongozi wa mkoa huo kutamatisha ziara mkoa wa Njombe ya kujifunza na kuanzisha mkakati wa ushirikiano wa pamoja wa mapambano dhidi ya udumavu.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko,Februari 10,2025 ameweka wazi kuwa ili kufanikisha mapambano dhidi ya udumavu wameanzisha kamati maalumu ambayo itafanya kazi kila siku hadi pale udumavu utakapotoweka.

Akizindua kampeni hiyo katika ukumbi wa ofisi yake, Mrindoko ameeleza kila mwananchi na mdau yeyote anawajibu wa kutambua kuwa wanayo kazi ya kufanya ya kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo ili kuondosha tatizo hilo.

Amesema mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa ya nyanda za juu kusini inayoshuhudiwa kwa uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula ambacho ni nyenzo muhimu kwa wananchi kupata lishe bora na kuwa wenye afya imara.

Mrindoko amebainisha lengo ni kuondoa udumavu ambapo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alilotoa Julai 13,2024 wakati akihutubia wananchi mjini Mpanda.

Katika kufanikisha mkakati huo, Mrindoko ametoa agizo kwa Katibu Tawala wa mkoa huo kuanza kubainisha asasi za wadau wa ndani na nje ya nchi watakaoweza kusaidia mapambano dhidi ya udumavu hususani kuweka msingi imara wa upatikanaji wa fedha za kuwezesha mkakati huo muhimu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Albert Msovela, amesema ziara waliyoifanya mkoa wa Njombe imewawezesha kujifunza namna bora ya kuanzisha mkakati wa kupambana dhidi ya udumavu.

Msovela amesisitiza kuwa udumavu utatoweka mkoani humo kupitia mkakati huo mpya na kwamba jamii inawajibu wa kutoa ushirikiano bila hofu yoyote kwa kamati na wataalamu mbalimbali wa afya na lishe.

Vicenti Nkana, Moja ya mzee maarufu wa mkoa huo ameeleza kuwa suala la udumavu kwa wananchi linachangiwa na tabia ya mtindo wa maisha ya watu kupenda kula chakula bila kufuata utaratibu mzuri kama unaoshauliwa na wataalamu wa lishe.

Ili kuwa na jamii yenye afya njema na yenye maendeleo endelevu jamii inapaswa kupewa elimu sahihi ya chakula na jambo zuri la kufurahisha ni kwamba tayari mkoa umechukua hatua hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti za wataalamu wa afya za mwaka 2022 mkoa wa Katavi unaonyesha kiwango kikubwa cha udumavu wa watoto chini ya miaka 5 kwa asilimia 32.2 jambo ambalo sio zuri kwa moja ya mkoa kinara kwa uzalishaji wa mazao ya chakula.