November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kata 11 Igunga kujengwa minara ya simu

Na Lubango Mleka, Timesmajira online,Igunga.

Kata 11 za maeneo ya Mbugani Jimbo la Igunga mkoani Tabora zinatarajia kujengewa minara ya mawasiliano hivi karibuni ili kutatua changamoto ya mawasiliano kwa wakazi wa maeneo hayo ambao ni wafugaji na wakulima wa mazao mbalimbali ya biashara na chakula.

Mbunge wa Jimbo la Igunga Nicholaus Ngassa akihutubia wananchi katika Kata ya Mwamashimba baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata hiyo.

Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora Nicholaus Ngassaleo katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mfuko wa jimbo,nguvu za wadau, wananchi pamoja na yeye mwenye.

Ngassa amesema,Kata hizo zitapatiwa huduma ya mawasiliano ya simu ambapo Mei 13, 2023 serikali imesaini mikataba na kampuni kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu, halfa ya utiaji saini ilishuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Jimbo la Igunga tumepatiwa minara ya mawasiliano ya simu itakayojengwa kwenye vijiji vyetu vilivyopo katika Kata ya Igurubi kijiji cha Kalangale, Kata ya Isakamaliwa maeneo ya katikati ya Hindishi na Isakamaliwa, Kata ya Itumba kijiji cha Itumba, Kata ya Itunduru eneo la Itunduru, Kata ya Bukoko kijiji cha Mangungu,”amesema Ngassa na kuongeza kuwa

“Nyingine ni Kata ya Kining’inila maeneo ya katikati ya Iyogelo na Mwanyagula, Kata ya Kinungu eneo la katikati Mwamagobo, Mwandinhimiji na Kinungu, Kata ya Mbutu katikati ya Mbutu na Mwabakima, Kata ya Mwamashimba ni katikati ya Mwamashimba, Ijogoyha na Mwanyalali, Kata ya Nguvumoja katikati ya Nguvumoja na Mwanshoma na Kata ya Mtungulu maeneo ya Mtungulu,”.

Katika hatua nyingine Mbunge Ngassa ameahidi kuweka umeme wa jua katika zahanati ya Mwamashimba ili iweze kutoa huduma nyakati za usiku umeme unapokuwa umekatika, huku akiahidi kuendelea kutatua changamoto ya maji katika vijiji ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo ifikapo Desemba mwaka huu.

“Tunaishukuru serikali kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa wananchi wa Jimbo la Igunga kwenye kuboresha miundombinu ya kuichumi na huduma za kijamii, hivyo ninawaomba wananchi wa maeneo ya Jimbo la Igunga kutuamini kwani mpaka sasa tumeisha tekeleza miradi mingi ikiwemo shule hii ya sekondari iliyogharimu kiasi cha milioni 400.7, ujezi wa zahanati ambazo sasa zinatoa huduma na zina vifaa tiba vya kutosha,” amesema Ngassa.

Wananchi wa Kata ya Mwamashimba wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Igunga Nicholaus Ngassa hayupo pichani alipofanya mkutano wa hadhara leo Mei 20,2023 katika kijiji cha Mwamashimba.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Kata hizo akiwemo Emmanuel Mandi, wamempongeza Mbunge huyo kwa kutekeleza ahadi na ufuatiliaji wa miradi hiyo.

“Sisi tunampongeza Mbunge Ngassa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia kwa kuitekeleza vyema Ilani ya CCM kwa kutupatia miradi na kuisimamia kwa wakati, tumeona leo ametuhakikishia kupata minara ya simu, kumaliza tatizo la maji katika vijiji vilivyobakia ifikapo Desemba, ametuahidi kufuatilia barabara yetu kuu itokayo Shinyanga kuja Igunga kujengwa kwa lami” amesema Mandi.

Huku Diwani wa Mwamashimba kutoka chama cha CHADEMA Andrew Lutuja,amesema Mbunge ni aina ya Mbunge waliyekuwa wanamuhitaji katika jimbo la Igunga kwani anajitoa sana kufuatilia miradi ya maendeleo.

“Ona leo anajenga ofisi za chama chake na leo ametoa mifuko 20 kwa kila kata alizopita, kwa kweli ni mtenda kazi mzuri sana, “amesema.

Mbunge Ngassa anafanya ziara katika Kata nne katika jimbo la Igunga ambapo ameanza Mei 19.2023,anatarajia kumaliza ziara yake kesho Mei 21,2023 lengo ni kukagua miradi ya maendeleo inayojengwa na serikali ya awamu ya sita chini ya usimamizi wa Rais Samia.