Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
NAHODHA wa Timu ya Manispaa ya Kinondoni KMC FC, Juma Kaseja pamoja na David Brayson wameungana na wachezaji wenzao kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Azam FC utakaochezwa Novemba 21 kwenye uwanja wa Uhuru.
Wachezaji hao wamerudi kikosini baada ya kumaliza majukumu yao ndani ya Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambayo ilikuwa na kibarua cha kusaka nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2021).
Katika mechi hizo Taifa Stars ilipoteza mchezo wa kwanza wa ugenini kwa kuruhusu goli 1-0 huku wakitoka sare ya goli 1-1 na Tunisia katika mchezo wa marudiano uliochezwa juzi usiku kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Mbali na Kaseja, Brayson, wengine waliorejea kuungana na kikosi cha KMC FC ni kocha wa makipa wa timu hiyo, Fatuma Omary ambaye aliitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Wasichana chini ya miaka 17 (U-17) ambayo imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michiano ya COSAFA iliyomalizika mwishoni mwa wiki nchini Afrika Kusini.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Christina Mwagala amesema kuwa, kikosi chao kinaendelea vizuri na maandalizi ya mchezo huo kwani wanachokihitaji ni alama tatu ambazo zitawawezesha kupanda kwa nafasi kadhaa katika msimamo wa Ligi.
Amesema kuwa, bado mikakati ya benchi lao la ufundi ni kuhakikisha kuwa wanapambana katika kila mechi iliyo mbeye yao ili kupata alama tatu ambazo zitawarejesha katika nafasi bora zaidi.
“Kaseja, Brayson pamoja na kocha wetu wa makipa, Fatma Omary wamerejea kikosini kuungana na wenzao ambayo tayari walishaanza maandalizi ya mchezo wetu dhidi ya vinara Azam, ” amesema Christina.
Kwa sasa bado KMC inaendelea kuwakosa wachezaji wawili bado hawajarejea kambini ambao ni Kenny Ally ambaye alifiwa na Baba yake mzazi pamoja na Rahim Sheihe ambaye bado yupo katika majukumu ya timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania