January 14, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Karia kujitosa kugombea FIFA, ujenzi shule ya soka kuanza karibuni

Na Yusuph Digossi TimesMajira Online

WAJUMBE wa Kamati ya Utendaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wameridhia rais wa shirikisho hilo Wallace Karia kugombea moja ya nafasi za wajumbe wa Shirikisho la Soka ulimwenguni (FIFA) kutoka nchi zinazozungumza kiingereza.

Makubaliano hayo yamefanyika katika kikao cha kawaida cha Kamati ya Utendaji (TFF) kilichofanyika jana kwenye Hoteli ya Tanga Beach Resort.

Akitoa ufafanuzi juu ya yale yalipopitishwa katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred amesema kuwa, baada ya FIFA na CAF kutangaza nafasi mbalimbali za kugombea kwa kauli moja wajumbe hao walikubaliana kama nchi ni muhimu kupata mwakilishi kwenye nafasi hizo.

Amesema, ndani ya siku mbili zijazo watapeleka rasmi barua kwenye mamlaka zinazohusika ili kuonesha kweli wana nia ya kugombea nafasi hiyo.

“Rais wetu atakuwa miongoni mwa wagombea wa hizi nafasi kwani Afrika ina nafasi mbili hivyo Tanzania kupitia rais Karia tutakuwa miongoni mwa watu watakaosaka hizo nafasi katika vyombo vya kimaamuzi hivyo maamini kwa umoja wetu kama nchi tuungane kwani itakuw ani jambo kubwa kwetu kupata nafasi hii, ” amesema Kidao.

Mbali na kuridhia jambo hilo lakini pia Kamati hiyo imepitisha kuanzishwa kwa Shule ya Soka ‘TFF School of Football Management ‘ itakayohusiana na masuala ya Utawala wa Mpira wa Miguu.

Tayari kamati hiyo imeshapokea drafti ya kwanza ambayo ilikuwa ikifanyiwa kazi na wataalamu kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam na washauri wengine kutoka vyombo mbalimbali kazi ambayo ilikuwa chini ya Mwenyekiti Dkt. Jonas Toboroha na Sekretarieti ya TFF kuhakikisha kuwa wanatengeneza mitaala kazi iliyomalizika kwa zaidi ya asilimia 80.

Amesema, Kamati ya Utendaji kwa pamoja wamekubaliana kazi hiyo iendelee ili kukamilisha kwa wakati na kuweza kuomba kutambulika na NACTE.

“Tunaamini kuwa jambo hili litakuwa chachu ya kutatua changamoto nyingi zinazokabili mpira wetu hasa katika utawala ambapo tumekuwa na changamoto kubwa na baada ya jambo hili kukamilika huenda Tanzania tukawa kama si nchi ya kwanza basi miongoni mwa nchi chache ambazo zimeanzisha programu ya namna hii” amesema Kidao.