April 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kapinga :Vitongoji 82 Tarime vijijini kupelekewa umeme na mradi wa HEP IIB

Na Penina Malundo, Timesmajira

Vitongoji 82 ambavyo bado havijafikiwa na umeme katika Wilaya ya Tarime mkoni Mara vitapelekewa umeme kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B (HEP IIB) ambapo tayari zabuni ya kuwapata wakandarasi wa mradi huo imeshatangazwa na inatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, tarehe 22 Aprili, 2025 Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara aliyetaka kufahamu lini Vitongoji vyote vya Tarime, vitapata Umeme.

Amefafanua kuwa Jimbo la Tarime Vijijini lina jumla ya Vitongoji 500 ambapo vitongoji 225 tayari vina umeme, vitongoji 52 Wakandarasi wapo wanaendelea na kazi, na vitongoji 82 zabuni ya kuwapata Wakandarasi imetangazwa kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B (HEP IIB) na vitongoji 141 vilivyosalia vitaendelea kupelekewa umeme kupitia miradi ijayo.

Kuhusu mpango wa Serikali wa kuunganisha Umeme katika taasisi mbalimbali kupitia fedha za mradi wa Covid 19, Kapinga amesema tayari Serikali ilishaanza kutekeleza mpango huo ambapo mpaka sasa zaidi ya taasisi 3000 zimeshaunganishwa na umeme zikiwemo taasisi za Elimu, Afya, Dini, Migodi pamoja na visima vya maji.

Vilevile amesema kuwa Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imeendelea kuwapatia umeme wananchi kupitia miradi mbalimbali ya umeme.