December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira

Naibu Waziri wa Nishati,Judith Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga kufanya mapitio ya maeneo ya Vijiji ambayo yanalipishwa bei ya mjini kuunganisha umeme ili yaweze kulipa bei stahiki ya Vijiji ambayo ni shilingi 27,000.

Kapinga ameyasema hayo leo Novemba 05, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Bukoba Vijijini, Mhe. Samsung Rweikiza aliyetaka kufahamu Serikali inachukua hatua gani kwa wananchi wa Vijijini wanaolipia gharama ya kuunganisha umeme zaidi ya 27,000.

“Kwenye baadhi ya maeneo ambayo ni Vijiji na yamekuwa yakitozwa gharama ya shilingi 321,000, , namuagiza Mkurugenzi Mtendaji TANESCO kufanya mapitio ya maeneo haya”, Amesisitiza Kapinga

Aidha, kuhusu Serikali kupeleka umeme Vitongoji visivyokuwa na umeme Bukoba Vijijini, Kapinga amesema Serikali inaendelea kuunganisha vitongoji ambavyo havina umeme ambapo vitongoji 258 kati 515 vya Jimbo la Bukoba Vijijjini vimefikishiwa umeme.

Aidha, kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji 27 ambavyo havina umeme katika Jimbo la Bukoba Vijijini inaendelea kupitia miradi ya ujazilizi 2B na Mradi wa Kupeleka umeme katika Vitongoji Awamu ya Pili A (HEP IIA).

Akijibu swali Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro, Kunti Msangi aliyetaka kufahamu Serikali inafanya jitihada gani kuondoa tatizo la umeme mdogo maeneo ya Kigamboni, Kapinga amesema Serikali inaendelea na maboresho ya kItuo cha kupokea na kupoza umeme cha Mbagala kwa ufungaji wa transfoma yenye ukubwa wa MVA 120 ili kuimarisha upatikanaji wa umeme maeneo ya Kigamboni, Mbagala pamoja na ukanda wa Pwani.

“Transfoma imeshafika na Mkandarasi yupo site anaendelea na kazi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kila jitihada kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata umeme wa uhakika” Amesema Mhe. Kapinga

Akijibu swali la Mbunge wa Nanyumbu, Ally Mhata aliyetaka kufahamu ni lini Serikali italipa fidia kwa Wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu ili kupisha ujenzi wa njia ya umeme ya Grid ya Taifa., Mhe. Kapinga amesema katika Wilaya ya Nanyumbu, Wananchi 689 wanapisha ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa Kilovoti 220 kutoka Tunduru hadi Masasi.

Ameongeza kuwa taratibu za kuwalipa fidia wananchi waliopisha mradi zinaendelea ambapo jumla ya Shillingi billioni 1.95 zinatarajiwa kulipwa kwa wananchi hao.

Amesema kwa sasa Serikali inaendelea na taratibu za upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kulipa fidia wananchi hao wa Nanyumbu ambapo na kuongeza kuwa fedha zitakapopatikana wananchi watalipwa stahiki hizo kwa wakati.

Akiongelea kuhusu upelekaji wa umeme kwenye Vitongoji Kapinga amesema maendeleo ni hatua na Serikali inaendelea kutelekeza miradi ya kupeleka umeme kwenye Vitongoji Nchi nzima.