November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Constantine Kanyasu akipokea fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea ubunge Jimbo la Geita Mjini huku akikabidhiwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Geita, Mwinyiheri Baraza leo. (Picha na Mutta Robert).

Kanyasu achukua fomu kutetea Jimbo la Geita Mjini

Na Mutta Robert,TimesMajira Online, Geita

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu mapema leo amechukua fomu kutetea nafasi yake ya ubunge wa Jimbo la Geita Mjini.

Kanyasu alichaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Geita Mjini kwa mara ya kwanza mwaka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, jimbo ambalo ameliwakilisha kwa kipindi cha miaka mitano hadi mwaka huu.

Akizungumza katika viwanja vya ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita mara baada ya kuchukua fomu, Kanyasu amesema kuwa, amechukua fomu kuomba kuendelea kuwakilisha jimbo hilo kwa muda wa miaka mingine mitano ili kuendelea kuwakilisha wananchi na kutekeleza Ilani ya CCM.

Amesema kuwa, aliahidi kushughulikia changamoto za wananchi, lakini haziwezi kuisha kwa siku moja hivyo amechukua fomu ili kuomba chama kumteua kuendelea kutumikia wananchi wa jimbo hilo la Geita Mjini.

Katibu wa Wilaya ya Geita wa CCM, Mwinyiheri Baraza amesema kuwa, hadi leo wanachama wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania ubunge katika majimbo matatu ni 67.

Wilaya ya Geita inaundwa na majimbo matatu ambayo ni Jimbo la Geita Mjini ambalo lilikuwa linawakilishwa na Constantine Kanyasu,Jimbo la Busanda ambalo lilikuwa linawakilishwa na Laurensia Bukwimba na Jimbo la Geita ambalo lilikuwa linawakilishwa na Joseph Musukuma.