Na Martha Fatael, TimesMajira,Online,Moshi
KAMPUNI ya Kimataifa ya Utalii ya Zara, imeliomba Bunge kusaidia uhamasishaji na kampeni maalumu ya wananchi kupanda Mlima Kilimanjaro kama sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Saidi Mtanda, ambapo imepewa jina la “Twenzetu Uhuru Peak” na inafanyika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ofisa Habari wa Zara, Ibrahim Jama, amesema safari ya kupanda mlima huo inatarajiwa kuanza Desemba 4 hadi 9, mwaka huu.
Amesema kampeni hiyo pamoja na kupewa nguvu na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini imelenga kushirikisha kampuni, taasisi, Watanzania na watalii kwa ujumla.
Amesema kampuni ya Zara na Kinapa zimejipanga kumuandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai ili kuhamasisha ushiriki wa wabunge pamoja na baadhi ya wizara ili kukuza utalii wa ndani.
Akizindua kampeni hiyo, DC Mtanda ametaka Zara kushirikisha balozi zilizopo hapa nchini,watu mashuhuri na kwamba Serikali inaunga mkono kampeni hiyo.
“Binafsi ni miongoni mwa watakaopanda mlima Kilimanjaro, nimeongea na wakuu wenzangu wa wilaya za Hai,Rombo, Siha na Mwanga na wameahidi kuniunga mkono,nadhani Meya wa Manispaa ya Moshi,Juma Raibu atapanda,” amesema
Katika taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu wa Zara, Zainab Ansell, amesema kwa zaidi ya miaka 15 kampuni yake imeshiriki katika kusaidia Jeshi la la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupanda mlima huo na mwaka huu anatarajia wageni takriban 100.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa KINAPA, Angela Nyaki amesema miongoni mwa maeneo yatakayofanyiwa uhamasishaji ni pamoja na vyuo vikuu katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro,vyombo vya habari na viongozi wa dini.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi