November 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampuni ya NGASMAKE, T-PESA, wazindua ‘Lipa kwa Uhakika’


Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Rai imetolewa kwa wanunuzi wa huduma au bidhaa kupitia mitandao ya kibiashara inayopatikana nchini kutumia mfumo wa LIPA KWA UHAKIKA ambao unatoa usalama wa fedha zao kwa kuondoa utapeli na udanganyifu

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya T-Pesa, Lulu Mkudde wakati wa uzinduzi wa huduma ya LIPA KWA UHAKIKA ambayo Ina lengo la kuondoa kilio cha muda mrefu cha wanunuzi wa bidhaa kutopata bidhaa zao ilihali wanakua wameshafanya malipo.

Mkurugenzi huyo amesema kupitia mfumo huo wa lipa kwa uhakika, muuzaji atasubiri mpaka mnunuzi apate bidhaa yake ndio fedha iingie kwenye akaunti yake.

Aidha amesema mfumo huo utakua na faida kubwa kwa upande wa muuzaji na mnunuzi;

“Mfumo huu utakuwa na faida kubwa kwa mnunuzi, fedha zake zitakuwa salama hadi apate bidhaa au huduma yake, pia anaweza kurudisha malipo yake ikiwa bidhaa haijawasilishwa”Alisema Lulu na kuongeza kuwa

“Kwa upande wa muuzaji yeye pia atafaidika kwa uwepo wa mfumo huo ambapo atakuwa na uwezo wa uhakika wa malipo mara tu wanapowasilisha bidhaa au huduma na pia atakuwa na uwezo wa kupokea taarifa ya Malipo kwa njia ya meseji kabla hajatoa huduma”

Pia Mkurugenzi huyo amesema Tanzania inajivunia kutokana na uwepo wa miundombinu rafiki ya mawasiliano yenye uwezo mkubwa wa kutosheleza mahitaji ya watumiaji nchini ambapo T-Pesa imewezesha huduma hiyo ya LIPA KWA UHAKIKA kutokana na miundombinu yao kuwa salama ya Miamala ya kifedha;

“Kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano kumeleta mageuzi makubwa nchini katika kuharakisha maendeleo katika sekta mbalimbali, kiuchumi na kijamii, uwepo wa Internet umesaidia sekta hii kupiga hatua, hivi sasa unaweza kufanya biashara popote ale Duniani kiganjani mwako kwa kuuza na kununua bidhaa kupitia inteaneti, LIPA KWA UHAKIKA ni suluhisho la bishara yako”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Ngasmake LTD, Emmanuel Ngalya amesema biashara ya mtandao imekuwa na changamoto nyingi za kiusalama kwa mnunuzi na muuzaji, kumekuwepo na udanganyifu na utapeli katika biashara na pia mnunuzi kupata huduma/bidhaa isiyo na kiwango;

“Kutokana na changamoto hiyo ndio maana kampuni ya NGASMAKE imekuja na suluhisho ya kuja na mfumo rafiki na salama wa LIPA KWA UHAKIKA, utakaosaidia mnunuzi na muuzaji kuwa salama katika biashara za mtandaoni na kuondoa changamoto ya udanganyifu, utapeli na kupata bidhaa zisizo na kiwango”

Aidha Ngalya amesema wameweka mfumo wao vizuri kwa watumiaji, endapo wakipata changamoto yoyote ya aidha kukosa huduma basi anaweza kuwasiliana nao bure kupitia namba maalum ya kituo chao cha huduma kwa wateja 0800110137 au kurasa zao za mtandao wa kijamii.

Mfumo wa LIPA KWA UHAKIKA unavyofanya kazi, mnunuzi baada ya kununua bidhaa na kulipia kupitia T-PESA fedha hizo hazitoenda moja kwa moja kwa muuzaji bali zitahifadhiwa kwenye mfumo mpaka mnunuzi atakapopata bidhaa yake na kuthibitisha ni bidhaa yenyewe aliyoiagiza ndipo mfumo utaruhusu fedha hizo kwenda kwa muuzaji.