November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampuni, taasisi zilivyojadili njia kupunguza NCD kwa wafanyakazi

*Tumbaku, wimbi la vinywaji vya sukari lafunikwa

Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

KONGAMANO la kwanza la mwaka 2024 la mpango wa kuboresha afya za wafanyakazi ili kuongeza ufanisi maeneo ya kazi limefanyika Jijini Dar es Salaam katika mjadala uliohusu mpango wa kupunguza Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD) kwa ustawi wa biashara hapa nchini.

Mpango huu wa uboreshaji afya unalenga taasisi, mashirika na kampuni katika mijadala inayoleta ufumbuzi wa matatizo ya wafanyakazi kiafya ili kuvutia mazingira ya ufanisi kwenye nyanja mbalimbali, zikiwamo za ubunifu na malengo ya kiutendaji.

Kwa sababu hiyo, kongamano linajadili changamoto zinazokwamisha malengo ya taasisi kupitia NCD, hasa zinazoweza kukwamisha morali ya wafanyakazi kikali na kimwili.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA), NCD ni magonjwa yasiyo na vimelea ambavyo vinaweza kuyasambaza. Mfano ni magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa, kisukari, kuoza meno, magonjwa ya akili na mengine ya kurithi kama vile seli mundu.

Kongamano linakutanisha wadau wa NCD, viongozi wakuu wa taasisi na kampuni na kubadilishana uzoefu wa mambo muhimu ambayo sehemu za kazi hayana budi kudumishwa ili kuepuka magonjwa haya na kuleta ufanisi.

Taasisi na kampuni zilizoshiriki katika kuendesha mijadala hiyo ni ya Benjamini Mkapa (BMF), Chama cha Waajiriwa Tanzania (ATE), Mwananchi Comminications LTD (MCL), Hospitali ya CCBRT, Hospitali ya Hindu Mandal na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS).

Waandaaji wa kongamano ni Tawi la Tanzania la Shirikisho la Kiamataifa linalotekeleza mipango ya Umoja wa Mataifa (UN) hasa katika kudumisha haki za binadamu, kanuni za ajira, mazingira na kupambana na rushwa, (UN-GCNT) na ImpactAfya ambalo linajihusisha na harakati za afya njema kwa kila kiumbe hai na lina mafungamano na mashirika mengine yanayopigania mitindo bora ya imaisha kwenye maeneo ya wafanyakazi.

Waandaji wa Kongamano la kwanza la mwaka 2024 la mpango wa kuboresha maeneo ya kazi wakionesha nakala za taarifa zao za kufungua mkutano. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Global Compact Network, Marsha Macatta-Yambi pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa ImpactAfya Ltd, Bhakti Shah.

Shirika la Kukuza Upeo wa Kifikra (TAI) ambalo linajihusisha na malezi bora ya vijana ili kufanikisha mabadiliko chanya ya maisha ya jamii, nalo lilishiriki.

Kwa upande wa serikali, Wizara ya Afya inawakilishwa na Mkurugenzi Msaidizi ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha NCD na Ajali, Dkt. Omary Ubuguyu.

Kabla ya kuingia kwenye mambo ambayo kongamano hilo linajadili kuhusu NCD, ni vyema nikaanza kwa kugusia juu ya mambo 10, amabyo wataalamu wa NCD wanayaelezea kama amri kumi ambazo jamii ikizifuata kikamilifu magonjwa haya yatapungua au kukoma kabisa.

TANCDA imeainisha mambo hayo 10 kama dira ya elimu na mapambano ya NCD nchini. Katika muainisho huo, matano yanahusu ulaji; usitumie mafuta mengi kwenye vyakula, kutotumia chumvi nyingi, kula kwa kiasi, kuzingatia ulaji wa mlo kamili, kula vyakula halisi kama vile kutokoboa nafaka na kula matunda yalivyo badala ya kukamua juisi.

Mengine matano ni kushughulisha mwili kwa kuepuka tabia bwete, kuishi kulingana na uwezo na kipato, kulala mfululizo kwa muda usiopungua saa saba kila siku, kuepuka matumizi ya tumbaku na ulevi na kufanya uchunguzi wa NCD mara kwa mara.

Mambo ambayo yamejadiliwa kwenye kongamano hilo ni uepukaji wa tabia bwete, uchunguzi wa NCD wa mara kwa mara, kupunguza unywaji wa pombe na kuepuka ulaji usiofaa.

Mshehereshaji wa kongamano holo, Khalila Mbowe anaonekana mahiri kwa kuhamasisha suala la mazoezi na mara kadhaa anawanyanyua waliohudhuria kwa kuwafanyiza mazoezi mepesi ya viungo.

Mazoezi hayo yanaonekana ni muhimu hasa kwa wafanyakazi ambao hutumia muda mrefu ofisisni. Anatoa mbinu na mitindo mbalimbali ya kuchangamsha mwili mzima kwa kuhusisha mikono, kichwa, shingo, kiuno na miguu.

Dk. Ubuguyu anaeleza kuwa mtu kufa kwa NCD siyo jambo la kushangaza ila kinachosikitisha ni kuona watoto na vijana wakipoteza uhai kwa kasi. Akaonya kuwa mbambo yanayochochea hali hiyo ni unywaji wa pombe kipindukia, ulaji usiofaa na ajali mbalimbali.

wafanyakazi kwenye tumbaku

Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran akataka wafanyakazi wote nchini kujengewa mazingira Rafiki kiafya kama sehemu ya kuwajali na kutambua mchango wao wa kusukuma mbele malengo ya waajiri wao.

“Janga la Uviko 19 lilitoa fundisho kubwa kwa waajiri,” anaonya Suzanne akiwataka waajiri kujenga mazingira mazuri kiafya kwa wafanyakazi ili suala la NCD lisiwe sababu ya kurudisha nyuma maendeleo ya kampuni au taasisi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Hindu Mandal, Profesa Kaushik Romaia alielezea kuwa njia muhimu ya kukabiliana na NCD ni kufanya uchunguzi wa mara kwa mara kwa wafanyakazi.

Mkurugenzi mtendaji wa (UN -GCNT), Marsha Macatta-Yambi anaeleza kuwa tamasha hilo linalenga kuoanisha mipango ya kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) katika biashara hapa nchini ili kuwiana na vita dhidi ya NCD.

Mkurugenzi Mtendaji, ambaye piya ni mwanzilisi wa ImpactAfya, Bhakti Shah alisema kongamano hilo ni muhimu kwao na linapaswa kufanywa jukwaa la kampuni, mashirika na taasisi kujadili mapambano ya NCD ili kuweka mikakati ya pamoja ya kujenga mazingira bora ya afya sehemu za kazi kwa kutumbia mbinu za kisasa.

Katika zile amri 10 za mapambano ya NCD, suala la tumbaku halikuzungumziwa kabisa.

Hii ni wazi kwamba kuna wafanyakazi hutumia sigara na ugoro katika maeneo ya kazi kama kitu cha kuwaliwaza.

Kundi la wachambuzi wa mikakati ya kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD) kwa ustawi wa biashara. Kutoka kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mambo ya Afya GGML, Dkt Aalen Mtemi, Mkurugenzi Mwendeshaji Mkazi wa PATH, Amos Mugisha, Meneja Mkuu Deloite Tanzania, Scholastica Williams, Mkurugenzi Mkazi wa PharmAccess, Heri Marwa.

Vilevile wapo wafanyakazi ambao wakienda sehemu za starehe hutumia shisha, ambayo ni mchanganyiko wa tumbaku iliyoongezewa vionjo vingine vya kuvutia.

Jambo jingine ambalo halikugusiwa ni wimbi la vinywaji vya sukari ambavyo vinaongezeka kwenye soko kila siku kwa ladha na vionjo tofauti na kuwavuta watu wengi kuvitumia, hasa vijana. Wapambanaji wa NCD wamekuwa wakizungumzia wimbi hilo kama moja ya sababu inayochochea kuongoezeka kwa wagonjwa wa NCD hapa nchini.

Katika kusimamia hilo, TANCDA waliwahi kuiomba serikali kutoruhusu biashara za vinywaji vyenye sukari kama vile juisi kwa sababu tafiti zao zinaonyesha matumizi ya muda mrefu yanasababisha watumiaji kuugua NCD.

Si hivyo tu, bali hata matumizi ya tumbaku pamoja na kilimo cheke kimekuwa kikinyooshewa vidole kama moja ya mambo ambayo hayana budi kupigwa marufuku au kutungiwa kanuni za kuyadhibiti.

Mmoja wa wahudhuriaji wa kongamano hilo, ambaye hakutaka jina lake kutajwa, anasema: “Yawezekana tumbaku na vinywaji vya sukari havikuzungumziwa kukwepa mgongano wa kimaslahi kwa kuwa zote ni biashara na zimeruhusiwa kikanuni hapa nchini zifanyike.”

Anafafanua kuwa mwenye mamlaka juu ya biashara zinazofanyika nchini ni serikali na ni vigumu kampuni iliyokwenye uwanja wa biashara kuinyooshea kidole nyingine.

Anasema suala la pombe lilizungumziwa kwa sababu suala watu kunywa pombe halijakatazwa ili kanuni za serikali zinaonya unywaji kupindukia na kwenye mjadala lilijitokeza kwa namna hiyo.