Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),limesema limeruhusu kampuni binafsi zaidi ya 30 kujenga vituo vya gesi asilia iliyogandamizwa chini (CNG) kuwezesha matumizi ya gesi hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka TPDC,Ahmad Massa amesema hayo Jijini Dar es Salaam, alipofungua semina kwa waandishi wa habari wa mkoa huo kuhusu mafuta na gesi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo.
Amesema, serikali kupitia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, imekuwa kielelezo katika bara la Afrika na dunia kwa ujumla katika mapambano ya kupiga vita matumizi ya nishati chafu ya kupikia.
“TPDC kupitia gesi asilia ni mdau mkubwa katika kuhakikisha hili linawezekana kwa kuwa gesi asilia ni bora na rafiki kwa mazingira ambayo ni nafuu na bei yake haiathiriki na athari za siasa ya kijiografia na mabadiliko ya thamani za fedha duniani, hivyo TPDC kwa kushirikiana na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) wanaendelea na utekelezaji wa usambazaji wa gesi asilia katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani,”amesema.
Akizungumzia semina hiyo, Massa amesema shirika hilo limeona kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu na uelewa kwanza kwa waandishi wa habari kuhusu masuala ya mafuta na gesi, kwa kuwa mwandishi mmoja akipata uelewa anaweza kuelimisha sehemu kubwa ya Watanzania kwa kutoa taarifa sahihi kupitia chombo chake cha habari.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano TPDC, Marie Msellemu amesema, semina hiyo ni mwendelezo wa utaratibu wa shirika hilo kuwajengea uwezo wadau wao kuhusu masuala ya gesi na mafuta nchini huku akibainisha kuwa Waandishi wa Habari wakipata uelewa kwa kutumia kalamu zao itakuwa rahisi kufikisha ujumbe kwa wananchi kile kinachoendelea katika shirika hilo.
Aidha Shirika hilo (TPDC) limesema lina mpango wa kuuza gesi asilia katika nchi nne za jirani Uganda, Kenya, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Akibainisha hayo Massa amesema, “TPDC ina mpango wa kuuza gesi asilia katika nchi za jirani ambazo tayari Serikali ilishaingia makubaliano ya awali na nchi hizo ni Uganda, Kenya,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia ambapo gesi inaweza kufika kwa wateja kwa njia ya bomba ama LNG/ Mini LNG, ” amesema.
Pia ameeleza kuwa, TPDC tayari imetia saini mikataba ya ujenzi wa mitambo ya Mini LNG na kampuni za ROSETTA, Africa 50 na KS Energy, kukamilika kwa mitambo hiyo kutawezesha usafirishaji wa gesi asilia katika nchi cha jirani.
Massa amefafanua kuwa, hatua hiyo itaiwezesha nchi kuwa tegemeo la nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Pia amesema shirika hilo linakwenda kushiriki moja kwa moja katika sekta ya kilimo nchini kwa kutumia kiasi cha gesi asilia kilichopo kwenda kuzalisha mbolea ya Urea.
“Tunaamini kiwanda kitakachokwenda kujengwa kwa kushirikiana na wenzetu wa Kampuni ya ESSA kutoka Indonesia katika mkataba tuliotia saini Julai 31, mwaka huu, kitakwenda kuwa mkombozi katika sekta ya kilimo nchini, pia kitaliwezesha Taifa kuwa tegemeo la mbolea katika ukanda wa Kusini mwa Afrika,”ameongeza Massa.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote