Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Iringa
KAMPENI ya siku kumi ya msaada wa kisheria ya Mama Samia imezinduliwa mkoani Iringa ambapo wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika huduma ya msaada wa kisheria inayotolewa katika viwanja vya Mwembetogwa mkoani humo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada,amesema Serikali imedhamiria kuwasaidia wananchi katika masuala ya kisheria hasa wanaoishi pembezoni mwa Mkoa,ambao wamekuwa wakishindwa kupata haki zao kutokana nakukosa fedha za kuweka wanasheria.
Amsema kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususani katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala, na masuala yanayohusu haki za binadamu kwa ujumla.
Pia amesema kuwa utekelezaji wa kampeni hiyo unafanyika kwa kushirikiana na Wizara na taasisi za Serikali,asasi za kiraia,wanazuoni na wadau wa maendeleo huku lengo kuu la kampeni ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.
“Ndugu zangu wananchi wa mkoa wa Iringa niwasihi jitokezeni kwa wingi kupata huduma hii ya msaada wa kiseria, Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan anatambua kama kuna wananchi wanashida ya msaada wa kisheria lakini hawana uwezo wa kulipia ada ya huduma hivyo hubaki wakisononeka na haki zao kupotea,”amesema na kuongeza:
“Niwaombe ndugu zangu katika hizi siku kumi jitokezeni kwa wingi kupata huduma za kisheria na huduma hizi zitatolewa hapa hapa viwanja vya Mwembetogwa na huduma hii ni bure,”amesema Mstahiki Meya Ibrahim Ngwada.
Aidha,amesema huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa katika siku kumi za katika Halmashauri na Wilaya zote za Mkoa wa Iringa, hivyo Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na vijiji wanatakiwa kuwahamasisha wananchi wao kujitokeza kutatuliwa shida zao.
Akizungumzia kapeni hiyo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dk. Franklin Rwezimula,amesema kuwa kampeni hiyo inaratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ambayo ni maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuwafikia wananchi wasio na uwezo.
Rwezimula amesema,Wizara inatarajia kuwafikia wananchi wote na kuhakikisha wanapata haki na usawa kwa wakati ili kufikia adhima ya Rais Samia kuhakisha wananchi wapata huduma ya kisheria bure.
Amesema kuwa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, imezinduliwa katika mikoa saba na Mkoa wa Iringa ni Mkoa wa nane ambapo huduma hiyo itatolewa kuanzia Desemba 11 hadi Desemba 19 mwaka huu.
Rwezimula ametaja mikoa hiyo kuwa ni Dodoma, Manyara Ruvuma Simiyu Shinyanga, Njombe, Singida na Iringa,huku mikoa mingine itakayozinduliwa kampeni hiyo kwa wiki hii ni pamoja na Mkoa wa Mara, Morogoro na Songwe.
Aidha amesema,katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya kisheria kampeni hiyo imeanzisha madawati katika Halmashauri zote nchini,ambapo yatatoa huduma kabla ya na baada ya kampeni.
Sanjari na hayo katika kufikia lengo hilo, kampeni inaongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa jamii hususani haki za wanawake na watoto.
Vilevile kampeni hiyo inatoa huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu elimu ya sheria, masuala ya haki na wajibu na misingi ya utawala bora.
Matokeo ya muda mrefu wa Kampeni hii ni kuchangia katika kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususani wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi. Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kisiasa hapa nchini.
Kadhalika amesema, kampeni inalenga kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi za Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa.Pamojana kuongeza idadi ya watu wanaotoa taarifa za matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Kupunguza idadi ya migogoro na matukio yanayotokana na ukosefu wa uelewa wa sheria,kuimarisha uwajibikaji na uwezo wa taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali zinazotoa huduma za msaada wa kisheria.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma ya Msaada wa kisheria mkoani Iringa John Tweve amewataka wananchi kuwa na utaratibu wa kuzitafuta na kuzilinda haki zao,kwa kusoma vitabu pamoja na kufika katika vituo vinavyotoa msaada wa kisheria hususani katika viwanja wanavyotoa huduma watu wa kampeni ya msaada wa kisheria wa mama Samia.
Kampeni hiyo ilianza kutekelezwa jijini Dodoma April, 2023 baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
More Stories
GST,BGS zafanya majadiliano namna ya kuanzisha mashirikiano katika tafiti na kujengeana uwezo
Utekelezaji wa Mou Tanzania,Burundi waanza rasmi
Profesa Janabi ampongeza Samia kwa uwekezaji MNH