Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Tabora
TAASISI ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imezindua kampeni ya uanzishaji na uimarishaji madarasa ya kisomo cha Elimu ya Watu Wazima (EWW) ambayo itaanza kutekelezwa katika halmashauri na Mikoa yote nchini hapa.
Hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo Kitaifa imefanyika katika shule ya sekondari Magreth Sitta,wilayani Urambo mkoani Tabora.

Akizindua kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Paul Chacha, Mkuu wa Wilaya ya Urambo Dkt. Hamis Mkanachi,ameeleza kuwa katika karne hii, elimu ya watu wazima si suala la hiari tena bali ni hitaji la msingi katika kujenga taifa lenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
‘Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 17 ya Watanzania watu wazima sawa na watu milioni 10.4 hawana stadi 3 za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) na kwa Tabora asilimia 32 ya wakazi wake sawa na watu milioni 1.85 hawana stadi hizo,”amesema Dkt.Mkanachi.
Dkt. Mkanachi amebainisha kuwa takwimu hizi zinatoa wito kwa viongozi, watunga sera na jamii kwa ujumla kuchukua hatua za makusudi za kupanga mikakati ya muda mfupi na mrefu ili kuondoa changamoto hiyo kwa watanzania.
‘Hivyo amenuagiza Ofisa Elimu Mkoa huo,kwenda kuweka mkakati wa kufikia wananchi wote,wawahamasishe kujiunga na madarasa ya kisomo hicho ili kupunguza idadi ya wasiojua kusoma,kuhesabu na kuandika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Profesa Philipo Sanga, ameeleza kuwa kampeni hiyo ni muhimu kwani itasaidia kupanua wigo wa uwepo wa madarasa ya kisomo cha EWW hapa nchini.
Amesisitiza kuwa madarasa hayo yanatoa fursa kwa wasio na stadi za KKK kujumuishwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo hivyo kujenga jamii imara na yenye ustawi mzuri kiuchumi.
Profesa Sanga amebainisha kuwa wanatarajia kuanzisha vituo vya mafunzo ya stadi za KKK katika mikoa yote,hivyo ameomba wadau kuunga mkono kampeni hiyo ili kutimiza kwa vitendo dhana ya elimu bila ukomo.
Ofisa Elimu Mkoa wa Tabora,Upendo Rweyemamu, amepongeza TEWW kwa kuanzisha kampeni hii na kuja na mkakati wa kujengwa vituo vya mafunzo ili kusaidia watanzania waliokosa fursa hiyo ili waweze kujiendeleza.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi