January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamonga atoa ahadi zingine akihitimisha kampeni Ludewa

a David John, TimesMajira Online, Nyasa

MBUNGE wa Jimbo la Ludewa ambaye amepita bila kupingwa Joseph Kamonga amehitimisha kampeni zake katika kata zilizopo mwambao mwa Ziwa Nyasa huku wananchi wa kata na vijiji hivyo wakionyesha imani kubwa na Mbunge huyo mpya.

Kamonga amehitimisha kamepeni hizo kwa kuwahutubia wananchi wa vijiji na kata za Lipingu, Lifuma, Makonde, Lumbila, Kilondo ambao wameweka wazi kero yao kubwa kuwa ni miundombinu hivyo wanaamini jambo atakaloanza nalo ni kushughulikia kero hiyo hasa katika eneo la barabara za kuunganisha kata hadi kata kutokea Wilayani Ludewa.

Wakizungumza kwa niaba ya wananchi wao, Viongozi wa vijiji na Kata za Lumbila wamesema kuwa, mwambao mwa Ziwa Nyasa changamoto kubwa ni Zahati, vituo vya afya, miundombinu ya barabara, Shule kukosa madarasa ya kutosha, kero ya maji kwa akina mama hali inayopelekea kuleta migogoro na waume zao.

Kero zingine ni kukosa haki ya kupata mikopo kutoka kwenye Halmashauri, uvuvi bora wa kutumia maboti ya kisasa kwa usalama wa maisha yao hivyo wanachotamani kuona ni kutatuliwa kwa kero hizo.

“Tunaimani kubwa na Mbunge wetu Kamonga na kupitia yeye mwambao mwa Ziwa tutapata maendeleo makubwa na hii ni kutokana na historia yake ya kusaidia watu wake hasa akiwa Afisa Ardhi Wilaya ya Ludewa kwa miaka sita iliyopita, ” amesema mmoja wa viongozi kutoka Chanjali, Adorati Mwaitulo.

Akizungumzia changamoto na matarajio ya wananchi hao, Kamonga ambaye ameshazunguka kata zote 26 za Wilaya ya Ludewa amesema kuwa, anatambua deni kubwa alilonalo kwa wananchi hao hivyo atajitaidi kutumika kadri ya matarajio yao.

“Ndugu zangu wananchi kimsingi nina deni kubwa sana na mimi ahadi yangu kwenu ni kuwatumikia kwa nguvu zangu zote na mnitume mtakavyoweza kwani mmezungumza mambo mengi ambayo yanawasumbua na kukera hasa kwenye maeneo ya barabara, maji, umeme, elimu kwa maana madarasa na walimu wachache, lakini hata wahudumu wa afya kwenye Zahanati hivyo nimeyachukuwa na nitakwenda kuyafanyia kazi mara tu baada ya kuapishwa,” amesema Kamonga na kuongeza.

“Kikubwa ni kuona wananchi mmeonyesha imani kubwa na Chama Cha Mapinduzi na ahadi yenu ya kumpigia kura nyingi Rais Dkt. John Magufuli pamoja na Madiwani wa CCM, hivyo lazima tutumike kwa ajili yenu.”

Mikutano hiyo ya Mbunge Kamonga iliongozwa na Mwenyekiti wa Wilaya ya Ludewa (CCM)Stanley Kolimba, Edward Haule ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri mstaafu na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Ludewa, Mwenyekiti wa Kamati ya siasa Wilaya, Pascal Mgimba, Mwenyekiti wa wazazi CCM John Kiowi pamoja na Madiwani waliopita bila kupingwa na viti maalumu Katibu wa tawi la Kiseke, Anusiata Lukuwi.