May 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamishina TRA avitaka Viwanda viwili Mkuranga kulipa kodi inayostahili

Na Rose Itono,Timesmajira

KAMISHINA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda amekitaka Kiwanda Cha kutengeneza viatu Vya Plastiki maarufu ‘Yeboyebo’ Cha Dolin na Fujian Hexingwang kinachozalisha nondo vilivyopo wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani kuhakikisha vinalipa kodi inayostahili kuendana na uzalishaji wao

Akizungumza mwishoni mwa wiki mara baada ya kutembelea viwanda hivyo Kamishina Mwenda amesema TRA imebaini ukwepaji wa kodi kwenye viwanda hivyo

Amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania inathamini kwa kiasi kikubwa Uwekezaji wa wageni wanaokuja nchini kwa ajili ya kufanya Uwekezaji kwani umekuwa na faida kubwa kwa Taifa kwa kuwezesha ajira kwa watanzania, hivyo ameagiza waniliki wa viwanda hivyo kuhakikisha wanalipa kodi stahiki inayotakiwa kwa mujibu wa taratibu za kodi zilizopo nchini

” Kupitia wasamaria wema ambao ni watanzania wazalendo tumepata taarifa za viwanda hivi kutokuwa na rekodi sahihi ya bidhaa inazozalisha na kuuza hali ambayo tumejionea na kubaini kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa ukwepaji wa kodi ,” amesema Mwenda

Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo timu ya wafanyakazi wa Mamlaka itaweka kambi kwa muda wa mwezi mmoja ndani ya viwanda hivyo ili kuweza kutoa elimu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa wahusika na wafanyakazi wake sambamba na kuangalia ni kiasi gani cha upotevu kimepatikana kwa kutokuwa na rekodi sahihi za uzalishaji ili wamiliki waweze kuilipa.

” Timu ya wafanyakazi wa TRA itaweka kambi ya mwezi mmoja ndani ya viwanda hivyo kwa lengo la kutoa elimu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa wamiliki na wafanyakazi sambamba na kuangalia namna uzalishaji unavyoenda ili waweze kubaini kiasi gani cha upotevu kimepatikana ili wamiliki waweze kulipa,” amesema Mwenda

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda Cha Dolin Lin Zhuhua alikubalia na uamuzi wa Mamlaka hiyo na kusema yuko tayari Kupokea maelekezo kutoka kwa wafanyakazi hao sambamba na kupata elimu itakayotolewa juu ya ulipaji kodi

Hata hivyo naye Xu Xingda ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kiwanda Cha Fujian Hexingwang aliungana na Kamishina Mkuu wa TRA na kusema yuko tayari kupokea maelekezo kama wamiliki wenzake wa viwanda vingine ili kuendelea na Uwekezaji wake nchini