January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Olimpiki Afrika, TOC wasaini mmakubaliano ujenzi kituo cha michezo

Na Jumbe Ismailly, TimesMajira Online

KAMATI ya Olimpiki Afrika kwa kushirikiana na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) wamesaini makubaliano ya kujenga kituo cha kimataifa cha michezo kwenye eneo la Kijiji cha Sagarumba, Wilaya ya Singida.

Akisaini makubaliano hayo kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Singida, Raisi wa Kamati ya Olimpiki Afrika, Gulamu Rashid amesema kuwa, ujenzi wa kituo hicho utakapokamilika utakuwa na Viwanja vya ndani, Hosteli, Riadha, Kikapu, Netiboli pamoja na viwanja vya michezo ya watoto wadogo.

Kwa mujibu wa Rais huyo, katika kipindi cha miaka takribani 14 iliyopita, kituo kama hicho kinachotarajiwa kujengwa Mkoani Singida, kilitarajiwa kujengwa Kibaha au Bagamoyo lakini kwa bahati mbaya katika ziara zao wakiwa pamoja na wanaoshughulika na shughuli za ujenzi, hawakuweza kupata kiwanja.

Badala yake, bahati hiyo ya ujenzi wa kituo kama hicho ilikwenda nchini Zambia na Tanzania walilazimika kuikosa bahati hiyo kutokana na kutokuwa na eneo la kujenga kituo hicho.

“Tunaamini kabisa kwamba katika mwendelezo wa shughuli hizi tutafanikiwa katika kuhakikisha kwamba tutajenga kituo na tunakiita ‘Sports Complex’ ambacho kitakuwa na michezo mingi kwa pamoja ikiwemo Riadha, Kikapu, Netiboli na mingine,” amesema Gulamu.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt Rehema Nchimbi akimkaribisha Rais huyo wa Kamati ya Olimpiki Afrika amesema kuwa, kituo hicho pamoja na kufanyika kwa michezo mbali mbali lakini pia kitakuwa ni kituo cha mafunzo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Elia Digha ameweka wazi kuwa, eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha kimataifa lipo katika Kata ya Merya, Tarafa ya Ilongero, Wilaya ya Singida.

“Kituo hiki cha Kimataifa cha michezo kitakuwa na ukubwa wa hekari 29 kinatarajia kujengwa katika Kijiji cha Sagarumba, Kata ya Merya wilayani Singida na tunatarajia kinakuwa chachu ya kukuza zaidi shughuli za michezo katika mkoa wetu,” amesema Digha.