Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Kamati ya Mipango Miji, Ujenzi na Mazingira ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imejipanga kuhakikisha inamaliza changamoto za ardhi na ujenzi holela ambazo zimekuwa kero kwa wakazi wa manispaa hiyo kwa muda mrefu.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Buzuruga, Manusura Sadick,wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kwanza wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo.
Ambapo amesema kamati hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo migogoro ya ardhi, ujenzi holela na ugomvi juu ya maeneo ya ujenzi, lakini imejipanga kuhakikisha kila tatizo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Sadick amesema kipaumbele cha kwanza ni kuimarisha miundombinu ya barabara, akibainisha kuwa tayari wameandaa mpango mkakati wa kupata bajeti pamoja na kutumia vitendea kazi vilivyopo kama malori na greda ili kuboresha barabara katika Kata zote 19 za Manispaa ya Ilemela.
Amesema hatua hiyo itaenda sambamba na kutatua migogoro ya ardhi, kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi.
Ameeleza kuwa kamati itaanza na maeneo ambayo hayajapimwa, kwa kuwa kutopimwa kwa maeneo kumekuwa chanzo cha migogoro hasa migogoro ya mipaka.
Sadick amesema kukamilika kwa upimaji kutasaidia wananchi kupata hati, kutambulika kisheria na kuepuka mgongano wa umiliki.
Pia amesema kamati hiyo itashughulika na changamoto ya maeneo kuwa na hati mbili au zaidi, kwa kuwa wanaanzisha kanzidata ya maeneo yote ili kubaini uhalali wa hati na kuondoa udanganyifu.
Amefafanua kuwa watatembelea kila eneo lenye mgogoro ili kupata uhalisia, badala ya kusubiri taarifa ofisini pekee.
“Kila eneo ambalo lina mgogoro wenye hati tukutane ofisini,na sisi tutatembelea maeneo yote kama Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuhakikisha kama kinachozungumzwa ni kweli tukiwa tumefika eneo husika na tumeona uhalisia wake,”amesema Sadick na kuongeza:
“Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi kulipwa fidia kisha kuuza eneo hilo kwa mtu mwingine,ambapo kitendo ni wizi na ukorofi hivyo wenye tabia hiyo waache mara moja,”amesema Sadick.
Sadick amesisitiza wananchi kufuata taratibu za kupata kibali cha ujenzi kutoka halmashauri au kwa watendaji wa Kata na mitaa, ili kuepuka hasara na migogoro ya baadaye endapo watakiwa wamefanya ujenzi katika eneo la wazi au ambalo halistahili kwa ujenzi.
Ameonya pia kuhusu ununuzi holela wa viwanja, akieleza kuwa matapeli wamekuwa wakiwauzia wananchi maeneo ya wazi au yasiyoruhusiwa kujengwa.
Hivyo amewashauri wananchi kwenda Idara ya Ardhi ya Halmashauri ya Ilemela ili wataalamu wakague kiwanja, namba ya eneo na umiliki kabla ya kufanya manunuzi.
“Kamati tumejipanga kutafuta taarifa, kufuatilia kwa ukaribu na kufika maeneo husika tukiwa na wataalamu,viongozi,jirani na muhusika tukishirikiana pamoja ili kuhakikisha haki inatendeka na umiliki halali unarudishwa kwa wenye haki,”amesema Sadick.
Sanjaru na hayo Sadick ametoa rai kwa watumishi wa mipango miji na idara ya ardhi ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kutenda haki, kutokuwa sehemu ya chanzo cha migogoro na kuhakikisha wananchi wanapatiwa haki zao kwa usahihi.
Amesema yeyote anayelazimisha haki ambayo siyo yake hatapata, na mwenye haki atasimamiwa hadi apate.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi