November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya kutathmini hali ya uchumi wa wanahabari yaongezewa miezi sita

Kamati ya kutathmini hali ya uchumi wa wanahabari yaongezewa miezi sita

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

WAZIRI wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ,Nape Nnauye ameiongezea muda wa miezi sita Kamati ya Kutathmini hali ya uchumi wa vyombo vya habari na wanahabari.

Amesema kuwa hatua hiyo imekuja kutokana na kamati hiyo kuomba kuongezewa muda ili iweze kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi.

Nape ameyasema hayo jijini hapa leo,Mei 23 ,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari mbele ya kamati hiyo ambayo awalu ilikutana na Waziri na kuomba kuongezewa muda baada ya kuona kazi hiyo ni kubwa na muda kutotosha.

“Kamati imefanyakazi kubwa na nzuri lakini tasnia ya habari inachangamoto zake na changamoto hizo zinatatuliwa na mifumo na mifumo hiyo inatengenezwa na wataalamu pamoja na kamati hii,

“Natambua kazi iliyofanywa na wataalamu pia kuihakikishia kamati inafanya kazi nzuri lakini kama alivyosema mwenyekiti wa kamati kazi hii itasaidia hadi nje ya Tanzania hivyo ni vyema ikafanywa kwa ufanisi mkubwa kwa kushitikiana na wataalamu wa masuala ya habari,”amesema Nape.

Vilevile Waziri Nape ametoa wito kwa wadaiwa wote ambao wanadaiwa na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini kulipa madeni yao ili vyombo vya habari viwe na hali nzuri

Awali Mwenyekiti wa kamati ya kutathmin hali ya uchumi kwa vyombo vya habari na wanahabari ,Tido Mhando akitoa mrejesho wa kamati hiyo juu ya kinachoendelea amesema kuwa wameiomba serikali kuwaongezea muda kutokana na kazi hiyo kuhitaji utafiti zaidi .

Amesema kuwa walikuwa wamejipanga kukutana na waandishi wa habari ili kuzifanyia kazi zile Moduli nne ambazo wamepewa lakini wataalamu kutoka vyuo vikuu na TCRA wametupa tafiti mbalimbali walizozifanya na tumeona kuna mambo mengi na hata suala letu la uchumi wa vyombo vya habari haliishii tu kwenye mishahara bali hata mapato yanavyopatikana ili kuboredha maslahi ya mwandishi wa habari.

“Waziri alituambia tusiende pupa kwa haraka haraka tuangalie hili jambo linazingatia uhalisia wa nchi yrtu lakini alituambia tutumie weledi kuhakikisha tunalifanya jambo hili kwa usahihi na ametupa hatua gani tunaweza kuzifuata kuona jambo hili tunalitekeleza,” amasema Tido.

Aidha Tido amesema kuwa ifikapo Novemba mwakabhuu kama walivyoomba kumaliza kazi hiyo itakuwa imekamilika na wataikabidhi.

Kamati hiyo ilianza kazi rasmi Januari 23 ,2023 ikiwa na wajumbe tisa ikiongozwa na Mwenyekiti wake Tido Mhando na Katibu wake Gerson Msigwa ambapo awali ilipewa miezi mitatu lakini sasa hivi inatarajiwa kumaliza na kukabidhi kazi hiyo ifikapo Novemba mwaka huu ikiwa imekamilisha miezi 6 iliyoomba kuongezewa.