Na Mwandishi Wetu Timesmajira online.
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Serikali kwa kuanzisha Maabara ya Udhinishaji wa Vifaa vya Mawasiliano ya Kielektroniki ikiwa ni maabara ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso Machi 15, 2025 jijini Dar es Salaam wakati Kamati hiyo ilipotembelea Mradi wa Maabara ya Uidhinishaji wa Vifaa vya Mawasiliano ya Kielektroniki unaotekelezwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Kakoso ameitaka Serikali kuendelea kuunganisha mifumo ya TEHAMA ya kisekta ili vifaa vya mawasiliano vinavyoingia nchini viwe na viwango vinavyotakiwa kitaifa, kikanda na kimataifa akitolea mfano wa mifumo ya TCRA na TBS kusomana.

Aidha, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeshauriwa kutoa elimu kwa umma kuhusu uwepo na umuhimu wa maabara hiyo ili kumwezesha mwananchi kufahamu ubora wa kifaa cha mawasiliano kabla ya kukinunua.
Pamoja na hilo Kamati imesisitiza kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza mara kwa mara kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali.
Akitoa taarifa ya maabara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabir Bakari amesema ujenzi wake ulianza mwezi Aprili 2023 na kukamilika Machi, 2024 ikiwa ni mwaka mmoja tu kama ulivyopangwa na inafanya kazi katika maeneo mawili ambayo ni eneo la kupima mawimbi ya redio na eneo ya kupima viwango vya mionzi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi ameishukuru Kamati na kuihakikishia kuwa Wizara imepokea ushauri wote uliotolewa na Kamati kwa ajili ya kuboresha.
Mhandisi Mahundi amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya mawasiliano na kusema kuwa Wizara itaendelea kuelezea mafanikio hayo katika Sekta ya Mawasiliano na TEHAMA.
Uwepo wa Maabara hii hapa nchini kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya 12 barani Afrika zenye maabara kama hii. Nchi hizo ni Tunisia, Afrika Kusini, Ghana, Nigeria, Cameroon, Benini, Togo, Senegal, Mali na Mauritania.
More Stories
CPA.Kasore ateta jambo na Riziki Ndumba,Mhitimu wa Fani ya Ushonaji, Ubunifu na Teknolojia ya Nguo
Serikali kuzindua Sera ya Ardhi ya 1995 Toleo la 2023
Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kuanzisha matibabu ya upasuaji moyo