Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC)limepongezwa na Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi, Mawasiliano, Ardhi na Nishati Zanzibar kwa utendaji kazi madhubuti katika usimamizi wa bandari na bandari kavu hapa nchini pamoja na usimamizi wa sheria na kanuni za usalama, ulinzi na utunzaji mazingira wa usafiri majini.
Akizungumza wakati wa Kamati hiyo ilipotembelea Ofisi za TASAC mkoani Tanga na kufanya kikao na watumishi wa TASAC pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA),Mwenyekiti wa Kamati,Yahya Rashida Abdulla amewapongeza watumishi wa ofisi hiyo kwa utendaji kazi katika Bandari hiyo na kupata matokeo chanya yenye maslahi mapana kwa Taifa.
Amesema kamati imefurahishwa na utendaji huo katika udhibiti na usimamizi wa safari kwa njia ya maji hasa katika Bandari ya Tanga ambayo kwa kiasi kikubwa imerahisisha usafiri kati ya Tanzania Bara na Visiwani.
Abdulla amesema kwa ufanisi huo TASAC imepata mafanikio makubwa kwani kwa sasa meli zinaweza kutoka Tanga hadi Zanzibar bila kupitia Dar es Salaam.
“Nimefurahishwa sana kuona sasa abiria wanaweza kufanya safari toka Zanzibar kuja Tanga bila kupitia Dar es Salaam, kwa hakika ni mafanikio makubwa sana. Hivyo niwapongeze sana kwa hatua hizi zilizopigwa na mamlaka hizi mbili TASAC na TPA,” ameongeza Abdulla.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu TASAC, Meneja Mafunzo na Utoaji vyeti , Lameck Sondo ameishukuru Kamati hiyo na kuahidi kuendeleza weledi, ufanisi na mashirikiano katika kudhibiti shughuli za usafiri majini kwa maslahi mapana ya Taifa.
Sondo ameongeza kuwa TASAC inaendelea na utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa usalama wa usafiri katika Ziwa Victoria (Multinational Lake Victoria Maritime Communications and Transport (MLVMCT) project) ambao ni mradi wa ushirikishwaji wa nchi za Uganda na Tanzania katika kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema kuwa Serikali kupitia TASAC imeendelea na ujenzi wa kituo kikuu cha uratibu wa masuala ya Utafutaji na Uokozi (Maritime Rescue Cordination Centre – MRCC) katika Ziwa Victoria ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 67.
Aidha, ameelezea kufanikiwa kwa hali ya juu katika ukaguzi wa meli za kigeni, pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara ya kuwajengea uwezo watumishi wake katika kutekeleza majukumu hayo ya kiudhibiti.
More Stories
Watendaji wa uboreshaji Tanga, Pwani watakiwa kufuata sheria kuhamasisha wananchi
Wiki ya Sheria yatambua mchango wa Majira, TimesMajira Online
Rais Samia kupokea Tuzo ya ”The Gates Goalkeepers Award”