November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yataka viongozi wa ushirika wasio waaminifu kuchukuliwa hatua 

Martha Fatael, TimesMajira Online

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara,Kilimo na Mifugo imetaka hatua za haraka kuchukuliwa dhidi ya  viongozi wa ushirika wasio waaminifu ili kunusuru sekta ya Ushirika  nchini hapa.

Pia kamati hiyo imebariki kuanzishwa kwa benki ya Ushirika nchini, ambayo waliitaka menejimenti yake itakapokamilika kuhakikisha inajiendesha kibiashara na kuepuka hasara kama miaka iliyopita.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mariam Ditopile Mzuzuri amesema hayo Aprili 22,2024 wakati kamati ikikagua hatua za uanzishwaji wa Benki ya Ushirika nchini itakayokuwa na makao makuu jijini Dodoma.

Amesema awali benki hiyo ilipita katika hali mbaya na kufikia kufilisika kutokana na uongozi mbovu wa menejimenti uliokuwepo.

Nao wajumbe wa kamati hiyo, wametoa maoni na kutaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote walioifirisi benki hiyo.

Wakichiangia baada ya kupokea taarifa ya benki hiyo, baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo waliitaka serikali kuchukua hatua za haraka kunusuru ushirika nchini kwani unashindwa kuwasaidia wakulima kutokana na kuwa na baadhi ya viongozi  wezi, wabadhirifu na wabinafsi.

Akitolea mfano, Mbunge wa Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi amesema benki hiyo ya KCBL awali ilikufa kwa sababu ya uwepo wa   baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu.

“Tunaomba kupata taarifa kamili kati ya watumishi wale waliosababisha  benki hii kufa, wamechukuliwa hatua gani za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.,” amesema Ndakidemi.

Katika taarifa yake Meneja wa KCBL, Godfrey Ng’ura amesema kwa sasa wamejipanga kuendesha benki hiyo kibiashara zaidi kuliko mwanzoni ingawa pia wanashirikiana na benki ya CRDB katika kuboresha huduma hizo kuwa za  kidigitali.

Amesema benki hiyo imeweza kutoka kwenye hasara kubwa na sasa inaendelea kukua jambo ambalo litaenda kuwanufaisha wanaushirika nchini.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema mafanikio ya benki ya Ushirika yatakwenda kuwainua wakulima wa mazao mbalimbali ambao awali walikosa sifa za kukopeshwa na benki nyingine nchini.

Benki hiyo ni muungano wa Benki za Kilimanjaro Cooperative Bank (KCBL) na nyingine ni Tandahimba Cooperative Bank.