June 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yaridhishwa na Mradi wa JNHPP

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesema imeridhishwa na maendeleo ya uzalishaji wa umeme katika Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere, ambacho kwa sasa kinachangia asilimia 45 ya umeme unaoingia katika Gridi ya Taifa.

Akizungumza leo, Juni 29, 2026, mara baada ya kutembelea Kituo hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Subira Mgalu, amesema Kamati imejionea kazi kubwa na ya kihistoria iliyofanyika katika ujenzi wa Kituo hicho pamoja na mchango wake mkubwa katika kuhakikisha Taifa linapata nishati ya umeme ya uhakika.

Mgalu amempongeza Rais.Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha Kituo hicho ambacho ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika kwa uzalishaji wa umeme kinakamilika na kuwa sehemu ya kichocheo muhimu cha upatikanaji wa nishati ya umeme inayochangia maendeleo ya nchi kijamii na kiuchumi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kukamilisha miradi ya njia za kusafirisha umeme, hususani mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Zuzu, Dodoma, ambao utawezesha usambazaji wa umeme hadi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa,ambayo ni maarufu kwa shughuli nyingi za uchimbaji wa madini.

“Kazi kubwa imefanyika katika Kituo hiki . Tunampongeza Rais kwa uwekezaji na kuhakikisha Kituo kinakamilika na mchango wake umeonekana katika uzalishaji wa umeme, sasa Kamati inashauri miradi ya njia za kusafirisha umeme inakamilika kwa wakati ili wananchi waendelee kunufaika na huduma ya umeme ya uhakika,” amesema Mgalu.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mha. Christopher Bitesigirwe, amesema Wizara kwa kushirikiana na TANESCO itaendelea kuhakikisha mitambo yote inafanya kazi kwa ufanisi na kuongeza jitihada za kukamilisha miradi ya njia za kusafirisha umeme.

“Leo tumepokea ugeni kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Kamati imejionea jinsi mitambo yote tisa inavyofanya kazi kwa ufanisi bila hitilafu yoyote. Tutayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa, hususani ya kukamilisha miradi ya njia za kusafirisha umeme,” amesisitiza Mha. Bitesigirwe.

Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO anayeshughulikia Uzalishaji, Mha. Antony Mbushi, amesema Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere kinaendelea kuzalisha umeme kwa ufanisi kwa manufaa ya Taifa, huku TANESCO ikiendelea kukisimamia na kuhakikisha mitambo inafanyiwa matengenezo kwa wakati ili kiendelee kutoa huduma bora.

“Kituo cha Julius Nyerere kinaendelea kufanya kazi vizuri. TANESCO itaendelea kukisimamia kwa karibu ili kuhakikisha uzalishaji wa umeme unaendelea kwa ufanisi na umeme unaozalishwa unasafirishwa na kusambazwa kwa wananchi kwa matumizi mbalimbali,”amesema Mha. Mbushi.

Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere kilikamilika rasmi mwaka 2025 na kina uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 2,115 za umeme, hatua ambayo imeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini na kuimarisha upatikanaji wa nishati hiyo muhimu.