Na Mwandishi Wetu
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Jerry W. Slaa imeona tija na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia TANESCO katika uwekezaji wa mradi mkubwa wa kusafirisha umeme kutoka Nyakanazi Kagera hadi Kigoma mjini wa kilovoti 400 kwa lengo la kufikisha umeme wa Gridi ya Taifa ambao utakuwa ni umeme wa uhakika na wenye ubora zaidi.
Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ziara katika kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme mkubwa cha Nyakanazi, Kagera Slaa (Mbunge) amesema,
“Kazi iliyofanyika hapa ni kubwa, tija ya uwekezaji imeonekana. Na sisi kazi yetu ni kuja kuona hizi pesa bilioni 654.29 ambazo nyingine zimetoka benki ya dunia, nyingine zimetoka African Development Bank, nyingine zimetoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani, nyingine zimetoka Mfuko wa Maendeleo wa Ufaransa (AfD) lakini nyingine zimetoka Serikali ya Tanzania. Fedha hizi zina tija kwenye uwekezaji? Na tija maana yake nini? Maana yake kama Kigoma, Kasulu, Kibondo walikuwa wanatumia majenereta ambao uzalishaji wake ni wa gharama kubwa, basi umetoka ule uzalishaji wa gharama kubwa umeenda umeme wa gridi ambao matokeo yake TANESCO inapata faida badala ya hasara kwa kuzalisha umeme kwa gharama nafuu”, alisema Slaa.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya TANESCO Mha. Abdallah Hashim kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo amesema, “Sisi kama Bodi tunahakikisha kuwa miradi hii yote yenye uwekezaji mkubwa sana tunaisimamia vizuri kila hatua na pia tunaitembelea miradi hii kuona tija (value for money)”.
More Stories
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini