November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yakutana na wafungwa,mahabusu Chato

Na Mwandishi wetu- GEITA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imetembelea Gereza la Wilaya ya Chato kwa lengo la kujionea namna mwitikio wa masuala ya UKIMWI unavyotekelezwa katika gereza hilo ambapo wamekutana na mahabusu, Wafungwa, Askari, Maafisa pamoja watumishi wa umma.

Akizungumza katika ziara hiyo Mkoani Geita Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus Nyongo amesema kamati imeridhishwa na jinsi Magereza inavyopanga na kutekeleza mikakati ya Mwitikio wa UKIMWI katika gereza hilo.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa afua za Mwitikio wa UKIMWI katika gereza la Chato zinaridhisha ambapo alimpongeza Mkuu wa Jeshi la Magereza kutokana na kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanakuwa salama kiafya.

“Nitumie nafasi hii kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani kila kinachofanyika ni kutokana na mwongozo na maelekezo yake. Pia niwasisitize kuchukua tahadhari ya maambukizi ya VVU ikiwa ni pamoja na kupima afya kwa wale ambao hawajapima ili mjue afya zenu, pamoja na kuanzishiwa dawa kwa wale ambao watagundulika kuwa na maambukizi ya VVU,”Amesema Mhe. Nyongo. 

Vile vile ameiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kuangalia namna ambavyo itaandaa mkakati maalum wa kutekeleza afua za UKIMWI katika magereza yote nchini ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo maafisa magereza katika utoaji elimu ya VVU katika maeneo yao.

“Niombe Ofisi ya Waziri Mkuu kama Mratibu wa masuala ya UKIMWI muangalie namna mtakavyo kuwa na mkakati wa kutekeleza afua za UKIMWI katika magereza nchini na kufanya magereza kuwa Mkoa wa kimkakati,ili kuhakikisha maambukizi ya VVU yanapungua pamoja na kuwawezesha Maafisa Magereza kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU,”

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga alieleza kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu inapokea maagizo yote yanayotolewa na Kamati hiyo kwa ajili ya Utekelezaji.

“Nilipongeze Jeshi la Magereza kwa kuendelea kutekeleza afua za Mwitikio wa UKIMWI pamoja na kuweka mikakati mizuri ambayo inalenga kumaliza UKIMWI ifikapo 2030,”Alipongeza Mhe. Nderiananga.

Kamati ilikutana na Mahabusu na Wafungwa ambapo katika risala yao wamebainisha changamoto zinazowakabili  na  baadhi ya changamoto zilipata utatuzi kutoka Machi kuisha  uongozi wa Jeshi la Magereza ikiwa ni pamoja na  kuwanunulia magodoro 50 kabla ya mwezi Machi kuisha , pamoja na kufanya utaratibu wa kuchimba kisima cha maji ili kupunguza changamoto  ya maji.

Kamishina Msaidizi wa Magereza Dkt. Richard Mwankina amesema kuwa elimu ya afya kuhusu VVU na UKIMWI hutolewa na watumishi wa afya waliopo gereza la Chato kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya, ambapo wafungwa na mahabusu wamekuwa wakifundishwa namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU na magonjwa ya ngono na kuepuka kuambukiza wengine .

“Kwa sasa jumla ya wafungwa na mahabusu 24 ndio wanaotumia dawa (ARV) na kuhusu elimu ya UKIMWI wafungwa na mahabusu wanapata habari na mafunzo mbalimbali wakiwa katika gerezani kupitia televisheni na vipeperushi ili kuongezea uelewa zaidi,”Amebainisha Dkt. Mwankina.

Awali Kamati ilitembelea hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato ambapo katika hospital hiyo pamoja na huduma nyingine inatoa huduma za tiba na matunzo kwa Watu Wanaoishi na VVU ambazo hutolewa kwa siku tano katika wiki kwa ajili ya kutoa dawa ,kuchukua vipimo ,ushauri na huduma nyingine.

Taarifa ya hospitali hiyo imeonesha kuwa katika mwaka 2023 jumla ya wateja 1253 walipima VVU ambapo wanaume walikuwa 682na wanawake 571, jumla ya watu 21 walibainika kuwa na maambukizi ya VVU pamoja kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU kwa kuhamasisha matumizi sahihi na endelevu ya kondomu kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Afya na masuala ya UKIMWI Mhe Stanslaus Nyongo amepongeza jitihada zinazofanyika katika kuimarisha huduma za afya na kuagiza fedha za miradi zinazotengwa zitolewe ili miradi inayoanzishwa isikwame.

Mwenyekiti ameielekeza Serikali kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya Afya zitolewe kwa wakati ili miradi hiyo isikwame, akisema uwekezaji huo ni mkubwa kwa kuwa itapunguza mzigo kwa hospitali ya moyo ya Jakaya Kikwete Dar es Salaam.