January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yajionea namna WMA inavyosimamia sekta ya mafuta bandarini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Oktoba 7, mwaka huu, imefanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam na kujionea pamoja na mambo mengine, namna Wakala wa Vipimo (WMA) wanavyosimamia sekta ya mafuta.

Meneja wa WMA Kitengo cha Bandari, Alfred Shungu amewaeleza Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Mariam Ditopile Mzuzuri kuwa majukumu yao huanza tangu mafuta yanaposhushwa kutoka Melini, kupitia kwenye ‘Flow Meter’ hadi kwenye maghala.

“Meli inapoingia, WMA hukagua nyaraka pamoja na kuhakiki mafuta yaliyoingia nchini ambapo baadaye takwimu hizo hulinganishwa na zilizopatikana katika ‘Flow Meter’ na kwenye maghala,” amefafanua Shungu.

Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Kitengo cha Bandari, Alfred Shungu (mwenye kizbao), akieleza majukumu ya Wakala hiyo katika usimamizi wa sekta ya mafuta kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, walipofanya ziara Bandari ya Dar es Salaam, Oktoba 7, 2024.

Akidadavua zaidi, amewaeleza Wabunge kuwa baada ya uhakiki, WMA huandaa taarifa na kuwapatia wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kukokotoa kodi.

Aidha, amesema kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), pia hukabidhiwa taarifa husika ili kujua kiasi cha mafuta yaliyoingia nchini na kwa upande wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) hupatiwa taarifa husika kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu.

Awali, akiwasilisha taarifa ya majukumu ya WMA kwa Kamati hiyo, Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi, Albogast Kajungu alisema mbali na usimamizi wa mafuta, Wakala hiyo pia hufanya ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa ikijumuisha za ndani ya nchi na zitokazo nje ya nchi kwa lengo la kumlinda Mlaji.

“Tunakagua bidhaa zilizofungashwa ili kujiridhisha ikiwa kile kilichoandikwa kwenye kifungashio ndicho haswa kilichomo ndani kwani wakati bidhaa hizo zinafungashwa, mteja anakuwa hayupo. Hivyo ni jukumu letu kukagua ili kuhakikisha mteja anapata kilicho stahiki,” amefafanua Kajungu.

Ameeleza majukumu mengine ambayo hutekelezwa na WMA ni pamoja na kuhakiki vipimo vya aina mbalimbali ikiwemo mizani, dira za maji, mita za umeme na vingine vingi, lengo kuu ikiwa ni kumlinda mlaji.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wakiwa katika ziara ya kazi, Bandari ya Dar es Salaam, Oktoba 7, 2024 ambapo pamoja na mambo mengine walijionea majukumu yanayotekelezwa na Wakala wa Vipimo (WMA) katika usimamizi wa sekta ya mafuta.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati, Mzuzuri amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Wakala wa Vipimo lakini pia amempongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri katika sekta ya biashara.

“Kwa niaba ya Kamati, tuchukue fursa hii kumpongeza sana Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji wake mkubwa sana katika sekta za uzalishaji, ikiwemo hii sekta ya viwanda na biashara.”

Ziara hiyo ya Kamati ya Bunge ilihusisha pia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na Tume ya Ushindani (FCC) ambapo Mwenyeji wa ziara hiyo alikuwa ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA), Albogast Kajungu akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Wakala hiyo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, ilipokutana na baadhi ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, Oktoba 7, 2024 jijini Dar es Salaam ikiwa katika ziara ya kazi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile Mzuzuri akiwaongoza Wajumbe wa Kamati hiyo katika kikao kazi na baadhi ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwemo Wakala wa Vipimo (WMA) Oktoba 7, 2024 jijini Dar es Salaam.