January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yaipongeza Wizara kwa maendeleo ya sekta yake

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Madini kutokana na mwenendo mzuri wa Ukusanyaji Maduhuli ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 pamoja na maendeleo ya Sekta ya Madini kwa ujumla ambapo mchango wa sekta ya hiyo kwenye Pato la Taifa umeendelea kuimarika.


Akitoa pongezi hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dunstan Kitandula ameitaka wizara kuhakikisha inafikia lengo ililopangiwa na Serikali pasipo kujiwekea doa. 
Katika Mwaka wa Fedha 2021/22, Wizara ya Madini imepangiwa kukusanya shilingi bilioni 650.

Aidha, Kitandula ameishauri wizara kuhakikisha inatekeleza kikamilifu masuala yote ya msingi ambayo yataiwezesha kutekeleza majukumu yake kikamilifu ili hatimaye Sekta ya Madini iendelee kutoa matokeo makubwa.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya  wizara kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 kwa kamati hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema kuwa, jumla ya shilingi 412,087,089,646.47 zimekusanywa na kuwasilishwa Hazina ambazo ni sawa na asilimia 95.09 ya lengo la kukusanya shilingi 433,340,001,333.33  katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Februari 2022.

Akizungumzia uimarishaji wa ukusanyaji  maduhuli na mchango wa sekta amesema kuwa, ili kuongeza maduhuli ya Serikali, wizara imeimarisha usimamizi  na ukaguzi kwenye maeneo ya uchimbaji, masoko ya madini, vituo vya uuzaji wa madini pamoja na mipaka ya nchi. Ameongeza kwamba, kutokana na juhudi mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali, mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kuimarika.

‘’Mhe. Mwenyekiti katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2021, mchango wa Sekta ya Madini umeongezeka hadi kufikia wastani wa asilimia 7.3 kutoka wastani wa asilimia 6.5 kwa kipindi kama hicho mwaka 2020,’’

Mbibo amesema mwenendo huo wa mchango unatoa mwelekeo chanya kuwa Sekta ya Madini itaweza kuchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo Mwaka 2025.

Akizungumzia biashara ya madini amesema, imeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka hivyo kuchochea ukuaji wa Sekta ya Madini. Amesema katika kipindi rejewa, madini yenye thamani ya jumla ya shilingi 5,657,650,059,362.06 yaliuzwa na Serikali ilikusanya kiasi cha shilingi 357,848,663,921.51 kama malipo ya mrabaha na ada ya ukaguzi.

Kwa upande wa  masuala ya leseni, amesema katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari 2022, wizara kupitia Tume ya Madini ilitoa jumla ya leseni 6382 ikilinganishwa na leseni 5,729 zilizotolewa katika kipindi kama hicho 2020/2021.

Akizungumzia usimamizi wa Masoko ya Madini, amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Februari 2022, mapato yatokanayo na mauzo katika masoko ya madini yaliongezeka kwa asilimia 12.4 ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021.

Amesema ongezeko hilo lilichangiwa na kuongezeka kwa idadi ya masoko na vituo vya ununuzi  wa madini kutoka masoko 40 na vituo vya ununuzi 58 hadi kufikia masoko 42 na vituo vya ununuzi 70.
Hayo ni miongoni mwa mafanikio machache ambayo yameainishwa hapa katika utekelezaji wa bajeti ya wizara kwa Mwaka wa Fedha 2021/22. 

Aidha, akihitimisha taarifa yake amesema, Sekta ya Madini imezidi kuimarika katika miaka ya hivi karibuni kutokana na  juhudi za makusudi zilizochukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuanzisha  na kusimamia masoko na vituo vya kuuzia madini katika maeneo yote yanayopatikana nchini, kudhibiti utoroshwaji wa rasilimali madini uliokuwa ukiendelea siku za nyuma, kuongeza weledi katika shughuli za uongezaji thamani madini pamoja na kutoa mafunzo, maelekezo na miongozo kwa wachimbaji wadogo kwa lengo la kufanya uchimbaji wenye tija.

Akitoa taarifa ya Tume ya Madini, Kaimu Katibu Mtendaji Mhandisi Yahya Samamba pamoja na mafanikio mengine yaliyotekelezwa amesema, jumla ya shilingi 501,233,895.65 ziliokolewa na kurudishwa Serikalini kutokana na udhibiti wa utoroshaji wa madini yaliyokamatwa. Ameyataja baadhi kuwa ni pamoja na madini ya dhahabu, vito, mchanga na madini ya viwandani yenye thamani hiyo.

Kwa upande wake, akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Nsalu Nzowa, ametaja baadhi ya mafanikio ya utekelezaji wa bajeti kwa shirika hilo kwa kipindi husika kuwa ni pamoja na kukamilika kwa miundombinu ya mtambo wa majaribio  wa uzalishaji wa makaa ya mawe ya kupikia  ambao umesimikwa na kuanza uzalishaji katika eneo la TIRDO mkoani Dar es Salaam. Amesema mtambo huo una uwezo wa kuzalisha tani 2 kwa saa na unatarajia kuliingizia shirika mapato ya shilingi milioni 742 kwa mwaka kwa kuanzia.

“ Mhe. Mwenyekiti, kwa sasa sampuli za makaa hayo zimepelekwa kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa ajili ya uthibitisho wa viwango kabla ya kusambazwa kwa walaji,’’ amesema Nzowa.
 Akizungumzia Mgodi wa Dhahabu wa STAMIGOLD ambao ni Kampuni Tanzu ya shirika hilo, amesema katika kipindi hicho cha Julai 2021 hadi Februari 2022, mgodi huo umezalisha wakia 7,106 za dhahabu na wakia 1,059 za madini ya fedha zote zikiwa na thamani ya shilingi bilioni 29.84.

Ameongeza kuwa, mgodi huo uliingizia serikali shilingi bilioni 2.09 kama mrabaha, ada ya ukaguzi na tozo mbalimbali pamoja na kutoa huduma kwa jamii inayozunguka mgodi.

Kwa upande wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Dkt. Mussa Budeba pamoja na mafanikio mengine ameileza kamati hiyo  kuwa ni pamoja  na GST kupata idhibati mbili  (2)  za njia  mbili za uchunguzi wa sampuli za madini.

Amezitaja njia hizo kuwa ni njia ya uchunguzi wa sampuli za dhahabu kwa njia ya Aqua Regia na upimaji wa kiwango cha majivu katika makaa ya mawe kwa njia ya gravimetric“’ Mheshimiwa Mwenyekiti, kupatikana kwa ithibati hizo kutakuwa na manufaa mengi kwa Taifa ikiwemo kupanua wigo kwa majibu ya uchunguzi unaofanywa na maabara ya GST kwa ajili ya uchunguzi na kuongezeka kwa makusanyo yanayotokana na huduma za maabara.’’ amesema Dkt. Budeba.

Naye, Kaimu Mtendaji wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) Mariam Mgaya, ameieleza kamati kuwa, thamani ya madini yaliyozalishwa katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 ilikuwa shilingi trilioni 4.7, thamani ambayo inaonesha ongezeko la asilimia 27 ikilinganishwa na Mwaka wa Fedha 2017/2018 ambapo thamani ya madini yaliyozalishwa ilikuwa shilingi trilioni 3.7.

‘’ Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa dhahabu ulikuwa asilimia 71.9 ya thamani ya madini yote yaliyozalishwa,’’ amesema Mariam.

Katika kikao hicho, wizara imewasilishwa na Watendaji na Wataalam kutoka wizarani na taasisi zake wakiwemo wenyeviti wa taasisi zilizo chini ya wizara.