Na Mwandishi Wetu
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakiongozwa na Mbunge wa Geita Mjini anayemwakilisha Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Constantine Kanyasu wako nchini Zambia katika ziara ya mafunzo kuhusu Uongezaji Thamani Madini.
Kanyasu ameambatana na wajumbe wengine watatu wa Kamati hiyo akiwemo Ndaisaba Ruhoro, Aleksia Kamguna na Janeth Mahawanga pamoja na Katibu wa Kamati, Chacha Nyakenga. Kwa upande wa Wizara, ujumbe huo unawakilishwa na Kamishna Msaidizi Sehemu ya Uongezaji Thamani Madini Archard Kalugendo.
Ziara hiyo, iliyoandaliwa na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia, ilianza Januari 12 na inalenga kuwapatia uelewa wabunge hao katika masuala ya uongezaji thamani madini na ushirikishwaji wa jamii nchini humo na inatarajiwa kukamilika Januari 16, 2025.
Leo tarehe Januari 13 2025, ujumbe huo ukiambatana na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Lt. Gen. Matthew Mkingule, umetembelea Wizara ya Migodi na Maendeleo ya Madini, nchini humo ambapo wamekutana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hapenga Kabeta na maafisa mbalimbali wa Wizara hiyo. Aidha, ujumbe huo umetembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia na kukutana na maafisa Ubalozi.
More Stories
ZOLA yajipanga kupeleka Nishati Safi kwa Watanzania, yaunga Mkono Juhudi za Rais Samia
Kiongozi wa Mwenge awataka RUWASA kukamilisha mradi wa maji kwa wakati Kilindi
Balozi Nchimbi aongoza waombolezaji kumuaga Mzee Mongella