Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga
KAMATI ya amani na maridhiano ya Mkoa wa Shinyanga kwa ushirikiano na wazee na machifu wa Mkoa huo wamelaani vikali matamko yanayoendelea kutolewa na baadhi ya wanasiasa wakipinga mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusiana na uendeshaji wa bandari.
Katika tamko hilo ambalo limesomwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Balulisa Khamis mbele ya waandishi wa habari limewataka wanaopinga uwekezaji huo wa bandari watumie lugha za staha na siyo kuwatukana viongozi wa kitaifa.
Wamesema baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitoa tafsiri potofu dhidi ya mkataba huo huku wakitumia lugha zisizokuwa na staha sambamba na maneno ya uchochezi yanayoweza kuondoa umoja wa kitaifa na kusababisha kutokea machafuko.
Wameendelea kufafanua kuwa, Serikali imetoa ruhusa kwa wadau mbalimbali kuendelea kutoa maoni yao na kwamba maoni hayo yatazingatiwa na kufanyiwa kazi lakini baadhi ya wanasiasa badala ya kutoa maoni yao wamekuwa wakitoa kauli chafu zisizokuwa na staha.
“Hivyo basi kupitia kikao chetu, tunatoa tamko kwamba, sisi Wazee, Machifu na viongozi wa kamati ya amani na maridhiano mkoani Shinyanga hatukubaliani, tunapinga na tunalaani vikali kitendo cha baadhi ya wananchi na wanasiasa kutumia lugha zisizokuwa na staha dhidi ya viongozi wa kitaifa,” amesema na kuongeza kuwa”
Katika hatua nyingine wajumbe wa Kamati hiyo wamewaomba wabunge na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuacha ukimya katika kuzungumzia suala hili badala yake waitishe mikutano ya hadhara kwa ajili ya kuwaeleza ukweli wananchi badala ya kuwaachia wapotoshaji waendelee kupotosha.
“Tuwaombe wawakilishi wetu na viongozi wa chama chetu tawala, waache kukaa kimya, wajitokeza kuwaelimisha wananchi juu ya suala hili muhimu kwa mstakabali wa taifa letu, hasa wabunge ambao wao wanalifahamu vyema na ndiyo waliolipitisha kule bungeni,”
“Kukaa kwao kimya kutasababisha maneno ya uongo yanayotolewa na baadhi ya wanasiasa na watu wengine kuonekana na ukweli mbele ya wananchi, tuwaombe sasa waitishwe mikutano ya hadhara katika maeneo yao ili kuwaeleza ukweli wananchi kuhusu suala hili la uwekezaji wa Bandari yetu,” ameeleza Sheikh Balulisa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Machifu mkoani Shinyanga, Chifu Charles Njange ameiomba Serikali ianze kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaotoa maneno yasiyokuwa ya staha dhidi ya viongozi wa Serikali hasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan.
“Tunaiomba Serikali sasa ianze kuwachukulia hatua watu wote wanaopotosha ukweli kuhusu suala hili, maana kutoa maneno yasiyokuwa na staha ni kosa la jinai, hivyo ni vyema sheria ichukue mkondo wake, matamko ya uchochezi yanaweza kusababisha kutokea vita ya wenyewe kwa wenyewe kama ilivyokuwa kwa nchi jirani ya Rwanda,” ameeleza Chifu Njange.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja