Na David John, TimesMajira Online
KAMANDA wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa amepiga marufuku magari yote ya mizigo pamoja na magari yanayokwenda nje maarufu kama IT kubeba abiria huku akitoa anyo kwa wamiliki ambao wanaingiza magari mabovu babaranani na kusababisha ajali.
ACP Mutafungwa ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa kufunga programu Maalum ya kutoa elimu ya Usalama Barabarani iliyopewa jina la Mahakama ya Watoto ya Kifani iliyofanyika katika Shule za msingi tisa za Serikali mkoani Dar es Salaam.
Amesema kuwa marufuku hiyo inaanza mara moja na itaenda sambamba na ukaguzi wa magari ambayo hayakuwekwa stika ya nenda kwa usalama barabarani nakuwataka kufika kwenye vituo vya polisi na stendi za mabasi kuhakikisha wanaweka stika.
Amefafanua kuwa kuhusu magari ya mizigo kubeba abiria amesema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya abiria au wamiliki wa magari hayo kubeba abiria na matokeo yake yamekuwa yakisababisha ajali, na kwamba jambo hilo ameshalikataza na katika operesheni iliyoanzishwa na Kikosi hicho watakamata magari yatakayobainika kubeba abiria wakati ni maalum kwa kubeba mizigo.
“Tukibaini gari ya mizigo (Lori) limebeba abiria tutalikamata gari pamoja na dereva na wamiliki wa magari hayo ,lakini hata magari yanayobeba abiria nayo ni marufuku kubeba mizigo.Tunataka watumiaji vyombo vya moto waheshimu sheria za Usalama barabarani ili kwa pamoja tushirikiane kupunguza ajali ambzo zinakatisha maisha ya Wananchi na wengine kubakia na ulemavu wa kudumu.
Nakuongeza kuwa “Kuhusu magari ya IT yanayosafirishwa kwenda nje za nje ya Tanzania nayo ni marufuku kubeba abiria na sheria inawataka kubeba abiria mmoja tu na si vinginevyo na hii haishii kwenye magari ya mizigo na IT tu bali hata magari yanayobeba magazeti nayo ni marufuku kubeba abiria.Katika hili hatutakuwa na utani, dereva na wamiliki lazima wafuate sheria za usalama barabarani,amesema Kamanda Mutafungwa.
Ameongeza kuwa iwapo abiria anataka kusafiri anatakiwa kwenda kwenye Vituo vya mabasi ya abiria ili kupata usafiri wa uhakika na unaotambulika kwa mujibu wa sheria.”Nasisitiza ni marufuku abiria kupanda gari ya mizigo,tutashukua hatua Kali.Tunakumbuka ajali ya gari iliyotokea Tanga watu watano walipoteza maisha na walikuwa wanasafiri na gari ya mizigo aina ya Fuso.”
Kuhusu makontena au mizigo ambayo haifungwi vizuri na kusababisha ajali amesema madereva na wahusika wanatakiwa kukahakikisha wanafunga mizigo ili kuwa salama wakati wote wa safari na kuongeza Jumatatu ya Aprili 4 mwaka huu yeye(Kamanda Mutafungwa) na maofisa wake watakutana na madereva waliopo Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuzungumza na kukumbushana wajibu wa kufuata Sheria za Usalama barabarani.
Akizungumza programu ya Usalama Barabarani iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Shirika la Amend Kamanda Mutafungwa alisema programu hiyo ni muendelezo wa kufikisha elimu ya Usalama Barabarani na kupitia programu hiyo Kuna madereva ambao watakuwa mabalozi wa wengine katika kuhamasisha kuzingatiwa kwa sheria za barabarani.
Kwa upande mgeni rasmi wakati wa kufunga programu hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate Mwegelo mbali ya kutoa shukrani kwa Shirika la Amend kwa kutoa mafunzo ya Usalama Barabarani kwa wanafunzi wa Shule za msingi ,alisema suala la ulasama barabarani ni jukumu la kila mwananchi na wote wanatakiwa kufuata sheria bila shuruti
Amesema kwa mujibu wa takwimu za Jeshi hilo zinaonesha kuwa kwa kipindi Cha mwaka 2021 watu 1245 walipoteza maisha yao na wengine 2, 023 walijeruhiwa kutokana na ajali za barabarani.”Kati ya takwimu hizo wanafunzi 56 walipoteza maisha na wengine 65 walijeruhiwa.Ni wazi kuwa jitihada zaidi zinahitajika katika kupunguza ajali na kundi ambalo liko hatarini ni wanafunzi ambao Shule zao nyingi ziko barabafani.
Ametumia nafasi hiyo kuliomba Jeshi la Polisi kuangalia namna ya kufanya kuhakikisha wanafunzi hawakai muda mrefu kwenye vituo vya daladala kwani madereva wengi wa daladala hawawapikii na hivyo wanafunzi kuchelewa kurudi majumbani.”Angalieni namna ya kuweka utaratibu ili madereva wa daladala wasiache wanafunzi vituoni.”
Pia aliwataka Wakala wa Barabara Tanzania ( TANROADS) na Wakala wa Barabara Vijijini ( TARURA) kuhakikisha barabara zinakuwa salama kwa watumiaji wote huku akisisitiza umuhimu wa kuwekwa kwa alama za barabarani yakiwemo maeneo ya shule.
Awali Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo akizungumzia programu ya Mahakama ya Watoto amesema lengo ni kuendelea kufikisha elimu ya Usalama barabarani kwa jamii ya Watanzani na wamekuwa wakitoa mafunzo hayo katika shule mbalimbali nchini.
Pia alisema uchunguzi unaonesha kuwa maeneo ya mijini na yanayoendelea zaidi ya asilimia tatu ya Watoto wanajeruhiwa kwa ajali za barabarani kila mwaka na zaidi ya asilimia 90 ya Watoto wanaoathirika ni wanaotembea kwa miguu huku akisisitiza Shirika lao litaendelea kushirikiana na wadau wengine katika kuifikisha elimu ya usalama barabarani kwa Watanzania.
More Stories
Mwinyi: Kuna ongezeko la wawekezaji Zanzibar
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi