November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiwanda cha Kairuki kuzalisha dripu nchini

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar es Salaam

NDOTO ya Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli imetimia baada ya kiwanda cha wazalendo kutangaza kuanza kuzalisha maji tiba (dripu) ambayo kwa miaka yote yamekuwa yakiagizwa nje ya nchi.

Kiwanda hicho cha Kairuki Pharmaceticals Industries Limited (KPIL) kinatarajia kuanza uzalishaji wake wa dawa mbalimbali Juni mwaka huu na kitakuwa cha kwanza kuzalisha maji tiba (dripu) hapa nchini.

Kwa sasa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) inaagiza maji tiba hayo kutoka nchi za Uganda, China na India

Mkurugenzi wa Hospitali ya Kairuki, Dkt. Muganyizi Kairuki ameiambia TimesMajira,Online juzi kuwa kiwanda hicho pia kitakuwa na maabara ya kisasa ya kuchunguza na kufanya tafiti za dawa mbalimbali.

Amesema kiwanda hicho kitatoa mafunzo kwa wanafunzi wa famasia na viwanda na kitakuwa na mifumo ya udhibiti wa hali ya hewa na mazingira ya ndani ya kiwanda .

“Kitakuwa na mitambo ya kisasa ya kuchakata maji tiba ambayo haijawahi kutokea hapa nchini kitakuwa kinatumia teknolojia ya kisasa kitakachofuata miongozo ya kimataifa GMP kuzalisha dawa inayotambuliwa na TMDA na Shirika la Afya Duniani (WHO),” amesema Dkt. Kairuki

Maji tiba

Amesema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha chupa za dawa 55,000,000 kwa mwaka na kutengeneza ajira za moja kwa moja 200 na ajira za muda zipatazo 500.

Amepotembelea Bohari Kuu ya Dawa (MSD),Rais wa awamu ya tano hayati Magufuli aihoji kwanini maji tiba hayo yanunuliwe nje ya nchi tena kwa bei ya juu miaka yote wakati kuna wataalamu wenye uwezi wa kuanzisha viwanda.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Meja Generali Gabriel Mhdize alisema iwapo kiwanda hicho kitaanza kuzalisha maji tiba ndicho kitakuwa cha kwanza kwa hapa nchini.

Amesema hiyo ni habari njema kwao kwani iwapo bidhaa hiyo itakidhi ubora unaotakiwa na kuthibitishwa na TMDA, MSD itakuwa inanunua hapo kwani kutakuwa na unafuu kulinganisha na kuagiza nje ya nchi.

Amesema MSD kwa sasa imeshaanza kuzalisha baadhi ya dawa tiba na za kupunguza maumivu lakini siku za baadaye itaanza na yenyewe kutengeneza maji tiba.