November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kairuki kufungua tamasha la wanawake

Na Queen Lema, Timesmajira online,Arusha

Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki anatarajiwa kufungua Tamasha la Wanawake (Wanawake Festival) litakalofanyika November 17 mwaka huu jijini Arusha ambalo litalenga kuwezesha kufikia idadi ya watalii milioni Tano ifikapo mwaka 2025.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Arusha Mwenyekiti wa tamasha hilo Nengasu Werema amesema kuwa wameamua kuunga mkono jitihada za serikali za kutangaza utalii.

Amesema kuwa watafanya tamasha hilo ambalo litashirikisha wanawake na wadau wa utalii kwa pamoja Ili kundi hilo liweze kushiriki kwenye sekta ya utalii.

“Tunataka kutangaza na kukuza sekta ya utalii kwani mada kubwa ya festival hii ni kuangalia namna ambavyo Wanawake wanaweza kujihusisha katika sekta ya utalii ambayo itawezesha kukua kwa uchumi wa taifa na wa mtu mmoja mmoja,”amesema.

Ameongeza kuwa katika tamasha hilo kutakuwa na tuzo mbalimbali ambazo zitatolewa kwa wanawake vinara wa utalii pia wataweza kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo ya Hifadhi ya Taifa Ngorongoro na Tarangire.

Kwa upande wake Ofisa Uhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire Jully Bede amewapongeza Wanawake hao kwa kuandaa tamasha hilo na kuahidi kuwapa ushirikiano ikiwemo kuwaeleza fursa zilizopo kwenye hifadhi.

Naye Mkurugenzi wa Wanawake na Utalii Mercy Michae amesema kuwa lengo la wao kuandaa tamasha hilo ambalo litashirikisha wanawake walioko kwenye sekta ya utalii ni kuhamasisha kundi hilo kuunga mkono sekta ya utalii na hatimaye kuweza kuongeza pato la taifa.