November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kagera yakamilisha miradi ya maji 73

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online. Kagera

MKOA wa Kagera umekamilisha miradi ya maji 73 yenye thamani ya sh. 62,516,688,102, hivyo kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi kutoka asilimia 42 iliyokuwepo mwaka 2015 katika miji, hadi kufika asilimia 65 iliyopo sasa na kwa vijijini kutoka asilimia 53 hadi asilimia 67.

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Warioba Sanya na kuongeza kuwa lengo ni kufika zaidi ya asilimia 85 kwa vijijini.

Amesema kwa miji ongezeko hilo ni kwa miji ya wilaya na mkoa, ambapo inatarajiwa kiwango cha upatikanaji maji kuongezeka kwa sababu ya uwekezaji katika miradi inayoendelea, akitolea mfano wa Manispaa ya Bukoba ambayo kwa sasa upatikanaji wa maji ni asilimia 90, itakayopanda hadi kufikia asilimia 95 ifikapo Juni 2021 baada ya mtandao BUWASA kuongezwa katika maeneo ya pembezoni.

Amefafanua kuwa kuna ujenzi wa miradi mikubwa ya maji mjini, inayohusisha ujenzi wa miradi ya maji katika mji wa Kayango wilayani Karagwe, mji wa Kyaka-Bunazi wilayani Misenyi, mjini Kemondo hadi Maruku wilayani Bukoba, mji wa Biharamulo na ujenzi wa mradi wa mifumo ya maji taka mjini Bukoba.