Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Kafiti Kafiti,ametoa wito kwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kushirikiana na wataalamu na wakuu wa idara,ili kutengeneza Ilemela yenye amani, maendeleo na uwajibikaji.
Wito huo umetolewa Novemba 2,2025 na Mbunge wa Jimbo la Ilemela,Kafiti Kafiti,wakati akizungumza katika mkutano wa kwanza wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,ambao umehusisha Madiwani kula viapo,uchaguzi wa Meya, Naibu Meya na wajumbe wa kamati za kudumu,kuunda kamati za kudumu za Halmashauri.

Pia kupitisha ratiba ya vikao vya halmashauri na kamati za kudumu pamoja na kupokea taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya utekelezaji wa shughuli za halmashauri zilizofanyika kipindi ambacho Baraza la Madiwani lilivunjwa.
Ambapo amewapongeza Madiwani wote wa Halmashauri hiyo waliochaguliwa huku akiwataka kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao.
Huku akisisitiza kuwa ushirikiano huo baina ya Mbunge,Madiwani na Wakuu wa Idara,usiwe wa kelele wala kuvutana,bali wavutane kwa maslahi ya Jimbo la Ilemela.
“Na tuvutane kwa staha,jambo ambalo litakuwa na kikwazo kikubwa nitalifikisha bungeni.Kabla ya kwenda Bungeni kwa kushirikiana na Madiwani na wataalamu tutakaa na kuona changamoto gani ambazo zimeshindikana na kunifikisha bungeni,”amesema Kafiti.
Kafiti amesema,lengo ni kuhakikisha miradi ya maendeleo inaenda mbele kwa kasi na wananchi wanaendelea kupata huduma bora.
“Tukishirikiana tutatengeneza Ilemela yenye maendeleo, amani na uwajibikaji,”amesema Kafiti.
Pia amesema wakati wa kampeni kilio kikubwa cha wananchi ilikuwa maji na miundombinu ya barabara.
“Changamoto hiyo ni kubwa,niwaombe sana Madiwani wenzangu na wakuu wa idara angalau kipaumbele chetu kiwe barabara na maji,”.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za halmashauri kuanzia Juni 20 hadi Oktoba 30, mwaka Mchumi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Herbert Bilia,amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026,halmashauri hiyo iliidhinishwa kupokea na kukusanya zaidi ya bilioni 86.89.

“Hadi Oktoba 2025, tumepokea na kukusanya zaidi ya bilioni 30.028, sawa na asilimia 35,kwa maana ya mapato ya ndani zaidi ya bilioni 4.9, sawa na asilimia 30 ya makisio,zaidi ya bilioni 3.3, sawa na asilimia 28 kwa ajili ya miradi ya maendeleo,”amesema Bilia na kuongeza:
“Huku zaidi ya milioni Shilingi 591 sawa na asilimia 39 kwa ajili ya matumizi mengineo na zaidi ya bilioni 21.1 sawa na asilimia 37 ni mishahara,”.
Bilia amesema, mahitaji ya watumishi katika Halmashauri hiyo ni 4,409 lakini waliopo ni 3,978 hivyo wanahitaji wa watumishi 431,hususani katika sekta ya ujenzi, walimu wa sayansi na watalaamu wa sekta ya afya.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi