December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kada wa CHADEMA Mdude sasa kuhukumiwa Juni 28

Na Esther Macha, TimesMajira,Online Mbeya

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mbeya, imeahirisha huku ya kesi inayomkabili, kada wa CHADEMA mkoani Mbeya, Mdude Nyagali, ambaye anatuhumiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya herioni.

Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Zawadi Laizer, alitoa uamuzi huo jana ambapo amesema sababu ya kuahirisha kwa hukumu hiyo ni kutokana kutokukamilika.

Kutokana na sababu hiyo amesema hukumu hiyo itasomwa Juni 28, mwaka huu huku akiahidi kuwa maandalizi yote ya kutoa hukumu hiyo yatakuwa yamekamilika.

Baada ya kuahirishwa kwa kesi nje ya mahakama Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amewaita wafuasi wa Chama hicho na kuwaomba kuwa watulivu wakisubiri Juni 28, mwaka huu kusikiliza hukumu ya mwanachama mwenzao.

“Hatuna budi kukubaliana na uamuzi wa mahakama kwa sababu ni suala lililo nje ya uwezo wao muhimu ni kusisitiza haki itendeke ili mwenzetu aaachiwe huru,” amasema Mbowe.

Kwa upande wake wakili upande wa utetezi, Faraji Mangula, amesema uamuzi wa Mahakama wameupokea kutokana na sababu zilizotolewa kwamba hukumu bado haijawa tayari hadi Juni 28, mwaka huu.

Amesema hawana pingamizi lolote na uamuzi huo na kwamba majukumu yao walishayamaliza kilichobaki ni kusikiliza hukumu ambayo inatolewa na Mahakama huku akiomba tarehe iliyopangwa hukumu itolewa bila kuwepo kwa sababu yeyote.

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe (kushoto) akisalimiana na kada wa chama hicho,Mdude Nyagali, kwenya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya jana kwa ajili ya kusikiliza hukumu ya kesi yake ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya herioni. Hukumu hiyo imeahirishwa hadi Juni 28, mwaka huu. Picha na Esther Macha.