January 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jumuiya za Chama zatakiwa kujiimarisha kiuchumi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

JUMUIYA za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora zimetakiwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali katika maeneo yao na kuisimamia ipasavyo ili kujiimarisha kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi alipokuwa akihutubia mamia ya wanaCCM na wakazi wa Kata ya Imaramakoye, Wilayani Urambo Mkoani hapa juzi katika maadhimisho ya siku ya wazazi Kimkoa.

Alisema jumuiya zote 3 ya Vijana, Wanawake na Wazazi ni kiungo muhimu katika kujenga chama hicho, hivyo zinapaswa kuanzisha miradi ya maendeleo na kuisimamia ipasavyo ili kujiimarisha kiuchumi.

Wakasuvi aliwataka viongozi wa jumuia hizo kuziimarisha kwa kuongeza  wanachama wapya, kutoa elimu ya malezi sahihi, kuitisha mikutano ya kikanuni na kikatiba na kutembelea wanachama wao.

‘Anzisheni miradi ya maendeleo, msipoteze muda kufanya mambo yasiyofaa, itisheni mikutano ya kikanuni na sio kushtukizana, yasemeeni mazuri yote yanayofanywa na serikali kwa wananchi’, alisema Wakasuvi.

Alisisitiza kuwa jumuiya imara ndio msingi wa chama imara, hivyo akatoa wito kwa viongozi kuziimarisha zaidi kiuchumi ikiwemo kudumisha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwao.

Wakasuvi alimpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake kubwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo, aliwataka Viongozi wa vyama vya siasa vyote kumuunga mkono kwa sababu maendeleo hayana chama.

Aidha aliwataka wabunge wa Mkoa huo kutokaa kimya bungeni bali waendelee kupaza sauti ikiwemo kuikosoa serikali kwa staha na dhamira njema ili kuharakisha maendeleo ya wananchi na kero zao kutatuliwa haraka.

Awali Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Tabora Eliezar Robert Kamoga aliwataka wanaCCM kushikamana na kuweka pembeni tofauti zao za uchaguzi uliopita ili kujenga jumuiya imara na Chama imara.

 Alisisitiza kuwa Jumuiya hiyo itaendelea kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vyote vya uvunjifu wa maadili miongoni mwa jamii na kutoa elimu ya malezi bora ili kujenga kizazi chenye maadili mema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi alikikabidhi kadi ya wazazi kwa mwanachama mpya wa Jumuiya hiyo Mzee Idd Kagete katika maadhimisho ya Jumuiya Wazazi yaliyofanyika Kimkoa katika Kata ya Imaramakoye, Wilayani Urambo Mkoani hapa Tabora juzi (Picha na Allan Vicent)