May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jumuiya za chama zatakiwa kuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kupitia Mkoa wa Tabora Mohamed Nassoro Hamdan (Meddy) ameahidi kuimarisha uhai wa chama katika Mkoa huo na kuwezesha jumuiya zake kuwa na uchumi imara.

Akiongea na gazeti hili Ofisini kwake jana alisema CCM ni chama kikubwa kilichobeba matumaini ya Watanzania hivyo katika kipindi chake cha miaka 5 atahakikisha kinakuwa imara zaidi na kufufua miradi ya kiuchumi ya jumuiya zote.

Alibainisha kuwa hana shaka na Chama chake katika nyanja ya kisiasa kwa kuwa kina wanasiasa waliobobea ila kinahitaji kusimamiwa vizuri ili kiweze kuwa imara zaidi katika nyanja 2 za kiuchumi na kisiasa.

Alisisitiza kuwa atahakikisha jumuiya zote 3 za Chama (UVCCM, UWT na Wazazi) zinakuwa na miradi ya uhakika itakayowaingizia kipato ili kufanikisha utekelezaji majukumu yao ya kila siku ikiwemo kuunganisha wanachama wao.

Aliongeza kuwa atatembelea wilaya zote 7 za Mkoa huo na kukutana na Viongozi wa Chama na Jumuiya ili kuwahamasisha kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao ikiwemo kuendeleza miradi iliyopo.

Meddy alifafanua kuwa wanaCCM wote wanapaswa kuwa kitu kimoja ili kuwa na chama imara hivyo akawataka kuweka makundi yao ya uchaguzi pembeni ili kudumisha umoja na mshikamano utakaofanya chama kiendelee kuaminiwa zaidi.

‘Uchaguzi umeisha, naomba wanaCCM wote turudi kujenga chama chetu, umoja na mshikamano wetu ndiyo silaha ya ushindi katika chaguzi zijazo, ule wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025’, alisema.

Alisisitiza kuwa mafanikio makubwa ambayo chama kimepata tangu kuanzishwa Februari 5, 1977 yametokana na umoja na mshikamano wa viongozi na wanachama, hivyo kudumisha mafanikio hayo hawana budi kuwa kitu kimoja.Aidha alisema atahakikisha Chama na Jumuiya zake zinakuwa na uchumi imara ili kufanikisha utekelezaji majukumu yao ikiwemo kutembelea wanachama wake na wananchi kwa ujumla ili kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Meddy alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji ilani ya uchaguzi ya chama ikiwemo kujenga chama imara.

Pichani ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (MNEC) kupitia Mkoa wa Tabora Mohamed Nassoro Hamdan (Meddy).