April 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jumuiya ya Wazazi yatakiwa kuhamasisha uchaguzi

Na Heri Shaaban, TimesMajira

Mjumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Taifa (viti 3 Bara) Dkt.Ally Mandai, amesema Jumuiya ya Wazazi ya CCM inahitaji kuendelea kuwa sehemu ya kutoa hamasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu kwani chama hicho kimejipanga kushiriki kikamilifu.

Dkt. Mandai ametoa kauli hiyo mkoani Mara wakati akihutubia wanachama wa CCM na Wananchi wa Musoma alipomwakilisha Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Ally Hapi, katika madhimisho ya wiki ya Wazazi kiwilaya.

“CCM imejipanga kikamilifu katika uchaguzi mkuu mwaka huu ili kuhakikisha inaendelea kushika dola,Jumuiya ya Wazazi ni injini ya kutoa hamasa na kutafuta kura kwa kushirikiana na Jumuiya zingine,” amesema Dkt. Mandai.

Amesema, Jumuiya hiyo itapita nyumba kwa nyumba, shina kwa shina kwa kushirikiana na Mabalozi wa mashina kuakikisha Chama cha Mapinduzi kinashinda kwa kishindo katika nafasi zote.

“CCM imejipanga kuendelea kuleta maendeleo kwenye taifa letu ili kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania,lakini Kuna watu wao vichwa vyao vimejaa makasiriko. chuki na maandamano,”amesema.

Hata hivyo amewasisitiza wana CCM kuwa na mshikamano, kuwashawishi wanachama bora watakaotatua kero za jamii kugombea nafasi za uongozi muda utakapofika.

“Kugawa fedha kwa wajumbe ili kushawishi kuchaguliwa siyo sehemu za sifa ya uongozi ndani ya CCM, na kuwa CCM ni ile ile yenye alama za jembe na nyundo hivyo sifa ya uongozi siyo rushwa bali uwezo wa kusimamia hoja za Wananchi waliokutuma kuwawakilisha na uadilifu,”.